1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Nani atashinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka 2023?

14 Septemba 2023

Zoezi la kupiga kura la kuchagua mchezaji na kocha bora wa mwaka 2023 limefunguliwa rasmi ikiwa ni siku chache tu baada ya FIFA kutangaza majina ya wachezaji na makocha walioteuliwa kuwania tuzo hizo.

https://p.dw.com/p/4WLyf
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi akipokea tuzo ya mchezaji bora wa mwaka
Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Argentina Lionel Messi akipokea tuzo ya mchezaji bora wa mwakaPicha: Michael Euler/AP Photo/picture alliance

Washindi wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya, Manchester City wanaongoza katika uteuzi wa wachezaji bora wa kiume wakiwa na wachezaji 6 kati ya 12 wanaowania tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa FIFA, kati ya hao ni mshambuliaji Erling Haaland ambaye ni mfungaji bora wa Ligi ya Mabingwa barani Ulaya msimu uliopita, beki Rodri, Julian Alvarez, Bernardo Silva, Kevin De Bryune na Ikay Gundogan aliyejiunga na Barcelona.

Wengine ni nyota wa timu ya taifa ya Ufaransa Kylian Mbappe na mshindi wa Kombe la Dunia Lionel Messi wa Argentina, Victor Osimhen, Declan Rice, Khvicha Kvaratskhelia na Marcelo Brozovic.

Soma pia: Hermoso akanusha kutoa ridhaa ya kupigwa busu na Rubiales

Pep Guardiola, Kocha wa Manchester City ambaye amebeba kila taji msimu uliopita katika ngazi ya vilabu yumo kwenye orodha ya makocha bora wa kiume akiwa na Luciano Spalletti aliyeiongoza Napoli kutwaa taji lao la kwanza la Serie A ndani ya miaka 33, majina mengine ni Simone Inzaghi, Ange Postecoglou pamoja na kocha wa Barcelona Xavi Hernadez.

Nyota wa timu ya taifa ya Ufaransa Kylian Mbappe
Nyota wa timu ya taifa ya Ufaransa Kylian MbappePicha: Robert Michael/dpa/picture alliance

Wachezaji bora kutoka Kombe la Dunia la wanawake mwaka huu wapo pia kwenye orodha ya wanaowania tuzo hizo za FIFA, mshindi wa Tuzo ya Mpira wa Dhahabu Aitana Bonmati na Jenni Hermoso aliyezua gumzo ulimwenguni baada ya kupigwa busu mdomoni na rais wa Shirikisho la Soka nchini Uhispania Luiz Rubiales ni miongoni mwa wachezaji wawili kati ya wanne wa mabingwa hao wa dunia wanaowania tuzo hiyo.

Washindi wa 2021 na 2022 wa tuzo ya kocha bora kwa upande wa Wanawake Emma Hayes na Sarina Wiegman wameteuliwa tena kushindania tuzo hiyo kwa upande wa wanawake.

Kwa upande wa makipa wanaowania tuzo ya golikipa bora wa mwaka ni Yassine Bounou wa timu ya taifa ya Morocco, Kipa wa Real Madrid Thibaut Courtois, Kipa wa Manchester City Ederson, Kipa wa Manchester United Andre Onana na Ter Stegen wa Barcelona.

Sherehe za Ballon d'Or mwaka huu zitafanyika Oktoba 30 mjini Paris, Ufaransa.