1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroSudan

Euro bilioni mbili zapatikana kwa ajili ya kuisaidia Sudan

16 Aprili 2024

Zaidi ya euro bilioni mbili za msaada kwa ajili ya Sudan zimechangishwa katika kongamano la wafadhili lililoandaliwa mjini Paris, Ufaransa. Rais Emmanuel Macron amesema kuwa hawajasahau kinachoendelea Sudan.

https://p.dw.com/p/4epAD
Sudan I Mzozo | Wakimbizi wa Sudan wakiwa kwenye foleni ya kupokea misaada ya kiutu.
Raia wa Suan waliokimbia vita vya wenyewe kwa wenyewe, wakiwa kwenye foleni ya kuchukua mahitaji ya msingi.Picha: Gregg Brekke/ZUMA/IMAGO

Hii ni baada ya Ujerumani, Ufaransa na Umoja wa Ulaya kuiomba jumuiya ya kimataifa kutoa msaada wa dharura kushughulikia hali ya kutisha ya kibinaadamu katika nchi hiyo inayokumbwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Rais Emmanuel Macron amesema wakati akiufunga mkutano huo jioni kuwa hawajasahau kinachoendelea Sudan. Amesema kiwango cha dhamira yao kitawawezesha kuyatimiza mahitaji ya dharura ya chakula, afya, maji, usafi, elimu na ulinzi wa watu walioko hatarini zaidi.

Waziri wa Mambo ya nje wa Ufaransa Stéphane Séjourné, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock, Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Joseph Borell na Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na Migogoro Janez Lenarcic walihudhuria mkutano huo, pamoja na wawakilishi kutoka asasi za kiraia nchini Sudan.

Guterres aonya kuhusu uhalifu wa kivita Sudan

Akizungumza mjini New York, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinaadamuhuenda umefanywa nchini Sudan. Alitaja mashambulizi ya kiholela yanayouwauwa, kuwajeruhi na kuwahangaisha raia wakati wamzozo huo kati ya jeshi na wanamgambo wa RSF.

Amesema ulimwengu unawasahau watu wa Sudan na kutoa wito wa juhudi za pamoja za kufikiwa mpango wa kusitisha mapigano na kumaliza umwagaji damu.

"Tatizo kuu liko wazi: kuna majenerali wawili ambao wameamua kuhusu suluhisho la kijeshi na hadi sasa, wanazuia juhudi zote kuu za upatanishi,” alisisitiza Guterres.

Amesema njia pekee ya kumaliza mzozo huo ni suluhisho la kisiasa. Vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan vimeingia mwaka mmoja tangu vilipoanza Arili 15 mwaka wa 2023.

Mwaka mmoja wa vita vya Sudan

Ujerumani yatangaza msaada zaidi kwa Sudan.

Mwanzoni mwa kongamano hilo, Baerbock alitangaza euro milioni 244 za ziada katika msaada wa kiutu kwa ajili ya Sudan. "Pamoja tunaweza kuepusha janga baya kabisa la njaa, lakini kama tutachukua hatua pamoja sasa,” aliongeza.

Soma pia: Wakimbizi wa Sudan wateseka Sudan Kusini

Kampeni hiyo ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa inahitaji dola bilioni 2.7 mwaka huu ili kupata chakula, huduma za afya na bidhaa nyingine za kuwapa watu milioni 24 nchini Sudan.

Mpaka sasa, wafadhili wametoa tu dola milioni 145 pekee, karibu asilimia tano, kwa mujibu wa ofisi ya masuala ya kibinaadamu ya Umoja wa Mataifa – OCHA.

Uingereza imeongeza maradufu msaada wake kwa Sudan nae neo Jirani hadi zaidi ya dola milioni 105 huku Marekani iliahidi dola milioni 100 za ziada. Halmashauri Kuu ya Ulaya inapanga kuahidi karibu dola milioni 355 kwa Sudan na mataifa Jirani katika mwaka wa 2024.