1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yatangaza msaada wa euro bilioni moja kwa Lebanon

Angela Mdungu
2 Mei 2024

Mkuu wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, ametangaza kuipa Lebanon msaada wa euro bilioni moja ili kusaidia kukuza uchumi wa taifa hilo.

https://p.dw.com/p/4fQCy
Rais wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya na Rais wa Cyprus ziarani Lebanon
Ursula von der Leyen (kushoto) akiwa na Rais wa Cyprus Christodoulides (katikati) na Spika wa bunge la Lebanon, Nabih BerriPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Von der Leyen ametoa ahadi ya msaada huo alipokutana na waziri mkuu wa muda wa nchi hiyo Najib Mikati mjini Beirut.

Ursula von der Leyen ametangaza msaada huo wa euro bilioni moja kwa Lebanon katika ziara yake nchini humo akiwa sambamba na Rais wa kisiwa cha Cyprus Nikos Christodoulides katika kasri la serikali mapema Alhamisi.

Von der Leyen amesema msaada huo wa kifedha utatolewa kuanzia mwaka huu hadi mwaka 2027. Ameongeza kuwa kupitia kitita hicho, Umoja wa Ulaya unataka kuchangia kuimarisha huduma za kiuchumi na kijamii za Lebanon.

Rais huyo wa halmashauri kuu ya Umoja wa Ulaya amefafanua zaidi kuwa fedha hizo zitatumika kuimarisha huduma za msingi kama vile elimu na afya.  Zaidi Von der Leyen amesema Lebanon inahitaji kasi nzuri ya kiuchumi ili kutoa fursa kwa biashara na raia wake.

Mkuu wa majeshi wa Lebanon, Joseph Aoun na waziri wa mambo ya kigeni Abdallah Bou Habib ni miongoni mwa waliohudhuria katika mkutano huo wakati msaada huo ulipotangazwa. Ahadi hiyo imetolewa wakati Lebanon ikikabiliwa na mgogoro wa wahamiaji na kitisho cha kutumbukia katika vita na taifa la Israel.

Hofu ya wakimbizi wa Lebanon kuingia Cyprus

Serikali ya Rais wa Cyprus Nikos Christodoulides inasema kuwa mashambulizi ya kujibizana kati ya Lebanon na Israel yamesababisha kuwepo kwa idadi kubwa ya boti zilizojaza wahamiaji kupitiliza wengi wao wakiwa raia wa Syria wanaokimbilia katika kisiwa hicho.

Ziara ya Ursula von der Leyen na Rais wa Cyprus nchini Lebanon
Rais wa Cyprus Nikos Christodoulides na Rais wa halmashauri kuu ya EU ziarani LebanonPicha: Hussein Malla/AP Photo/picture alliance

Awali Rais huyo aliitembelea Lebanon April 8 na kutoa ombi kwa Umoja wa Ulaya kuingilia kati na kuzuwia wakimbizi hao wanaotokea Lebanon kuingia nchini mwake.

Soma zaidi: Makabiliano yaongezeka mpakani mwa Israel-Lebanon

Lebanon, yenye zaidi ya wakimbizi 800,000 wa Syria wanaotambuliwa na Umoja wa mataifa imekuwa ikikabiliwa na mgogorowa uchumi tangu mwaka 2019. Kati ya wakimbizi hao, asilimia 90% wanaishi katika hali ya umasikini mkubwa.

Takwimu hizo ni kwa mujibu wa Shirika la Kuhudumia Wakimbizi la Umoja wa Mataifa UNHCR. Hata takwimu rasmi za Lebanon zinakadiria kuwa wakimbizi waishio nchini humo ni kubwa kuliko ya shirika hilo la kuhudumia wakimbizi ambayo ni kati ya watu milioni 1.5 hadi milioni 2.