EU yajitolea kuandaa kikosi cha kulinda amani Ukraine
12 Desemba 2024Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas amesema leo kuwa umoja huo umejiandaa kuratibu juhudi katika mwelekeo huo.
Amesema Umoja wa Ulaya utaendelea kuisaidia Ukraine kwa njia zote muhimu.
Shirika la habari la DPA limesema wawakilishi wa baadhi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO wamekuwa wakifanya mazungumzo ya siri wiki kadhaa kuhusu uwezekano wa kufikiwa makubaliano ya kusitisha vita siku zijazo nchini Ukraine, na jinsi yanavyoweza kufuatiliwa.
Aidha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Annalena Baerbock amesema Ukraine itahitaji msaada wa muda mrefu wa kijeshi na kifedha.
''Ukraine inahitaji kuhakikishiwa usalama, na sisi kama watu wa Ulaya tunapaswa kulitimiza hilo kwa dhati. Hii ni pamoja na msaada wa muda mrefu wa kijeshi na kifedha kwa Ukraine.''
Wasiwasi unaongezeka kwamba Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, anaweza kujaribu kuzishinikiza Ukraine na Urusi kufanya mazungumzo mara tu atakaporejea madarakani.