1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

EU yaidhinisha chanjo ya tano dhidi ya Covid-19

21 Desemba 2021

Umoja wa Ulaya umeidhinisha chanjo ya tano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19, na kuongeza kasi katika kukabiliana na kirusi cha Omicron kinachoikosesha dunia usingizi.

https://p.dw.com/p/44btM
Novavax
Picha: Tomislav Miletic/PIXSELL/picture alliance

Wakala wa dawa za Ulaya EMA umeidhinisha chanjo ya tano dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 wakati Marekani ikitahadharisha juu ya ongezeko la maambukizo mapya katika msimu wa baridi kali.

Jana Jumatatu, wakala hiyo iliidhinisha chanjo kutoka kwa kampuni ya dawa ya Marekani ya Novavax.

Soma pia: WHO: Omicron inasambaa kwa kasi zaidi ya Delta

Hiyo ni chanjo ya tano kuidhinishwa na Umoja wa Ulaya baada ya Pfizer, Moderna, AstraZeneca na Johnson & Johnson.

Tayari Umoja huo umetia saini mkataba wa kununua hadi dozi milioni 200 za chanjo hiyo ya Novavax.

Kampuni hiyo ya dawa ya Novavax imesema chanjo yake imeonyesha ufanisi wa asilimia 90.4 dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 wakati wa majaribio yake.

Pfizer, Moderna, AstraZeneca na Johnson & Johnson zimeidhinishwa tayari

WHO I Malaria I Director-General Tedros Adhanom Ghebreyesus
Mkurugenzi Mkuu wa WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus Picha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Wakati hayo yakiarifiwa, mkurugenzi mkuu wa shirika la afya duniani WHO Tedros Adhanom Ghebreyesus ametoa wito kwa mataifa duniani kuongeza juhudi za kusaidia kumaliza janga la Covid-19, akihimiza sherehe za mwaka mpya kufutwa akisema ni bora kusherehekea baadaye kuliko kusherehekea sasa na kuhuzunika baadaye.

Ghebreyesus amesema ulimwengu lazima uungane na kufanya maamuzi magumu ili kulitokomeza kabisa janga la Covid-19 kufikia mwaka ujao.

Mkurugenzi mkuu huyo wa shirika la afya duniani akiwa mjini Geneva, amewaambia waandishi wa habari. "Mwaka 2022, ndio mwaka wa kulimaliza janga hili, lakini pia ndio mwaka ambao nchi zote zinafaa kuungana ili kuzuia athari ya majanga kama haya katika siku zijazo."

Ghebreyesus amesema mataifa mengi yanapaswa kupunguza au hata kuahirisha hafla zenye kuvutia mikusanyiko mikubwa ya watu kuelekea likizo ya Krismasi na mwaka mpya, akitahadharisha kuwa sehemu zenye mikusanyiko ya watu ndio fursa nzuri ya kusambaa kwa kirusi cha Omicron.

Soma pia:Mataifa yajipanga kulazimisha chanjo ya corona kwa wote

Tangu kilipogunduliwa kwa mara ya kwanza nchini Afrika Kusini mnamo mwezi Novemba, kirusi cha Omicron kimesambaa kwa kasi katika sehemu mbalimbali duniani na kuzima matumaini kuwa janga la Corona lilikuwa linakaribia kuisha.

Licha ya kuwa mataifa ya Ulaya yamepiga hatua kubwa katika utoaji wa chanjo tofauti na sehemu nyengine duniani, lakini kirusi cha Omicron kimesababisha ongezeko la wagonjwa na kulazimisha baadhi ya mataifa duniani kurudisha vizuizi vikali ili kudhibiti kusambaa kwa kirusi hicho.