1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ethiopia yajiandaa kwa uchaguzi wa bunge

Coletta Wanjohi18 Juni 2021

Ethiopia inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa bunge unaofanyika Jumatau wiki ijayo, ambapo chama kitakachoshinda kitaunda serikali kwa kutoa waziri mkuu.

https://p.dw.com/p/3vBiA
Äthiopien Premierminister Abiy Ahmed Parlament
Picha: Yohannes Gebireegziabher/DW

Ethiopia inajiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa bunge unaofanyika Jumatau wiki ijayo, ambapo chama kitakachoshinda kitaunda serikali kwa kutoa waziri mkuu. Serikali ya sasa inayoongozwa na Waziri Mkuu Abiy Ahmed imeahidi  kwamba uchaguzi huo utakuwa huru na wa haki, lakini changamoto kadhaa zitawazuwia wananchi wengine kupiga kura. 

Tume ya Uchaguzi ya Ethiopia inasema imeweka mikakati ya kutosha kuhakikisha kuwa wananchi watakaopiga kura watafanya hivyo kwa njia halali na huru. Kulingana na tume hii, zaidi ya wananchi million 37 wamejisalili katika maeneo mbalimbali ya nchi.

Hata hivyo, kati ya majimbo 547, majimbo 110 hayataweza kushiriki katika uchaguzi huu wa tarehe 21.

Tume ya uchaguzi linasema kuwa maeneo mengine hayawezi kufikiwa kwa sababu ya ukosefu wa usalama, na mengine kwa ajili ya miundombinu duni na sababu ambazo haziwezi ruhusu vituo vya kupigia kura kuwekwa huko.

Kwa hivyo kutakuwa na awamu ya pili ya uchaguzi, yumkini katika mwezi Septemba kwenye maeneo hayo, likiwemo jimbo la kaskazini la Tigray, ambako vita baina ya jeshi la serikali kuu na la jimbo hilo vimempaka matope Waziri Mkuu Abiy Ahmed, ambaye pia anatafuta ushindi katika uchaguzi huu.

Soma zaidi:UN yaonya kuwa raia wa Tigray wanakabiliwa na kitisho cha njaa

Umoja wa Mataifa unasema zaidi ya watu milioni tano kwenye jimbo hilo wako katika hali mbaya na zaidi ya milioni moja wamelazimika kuyakimbia makaazi yao. Eneo zima la kaskazini linasemakana kuwa linahitaji usaidizi wa haraka.

Zaidi ya wananchi millioni 37 wamejisalili katika maeneo mbalimbali ya nchi

Äthiopien Konflikt in Tigray | Flüchtlinge in Sudan
Wakimbizi wa Ethiopia waliokimbia mapigano katika jimbo la TigrayPicha: Ashraf Shazly/AFP/Getty Images

Serikali ya Abiy Ahmed inajitetea kwa kukanusha ukosoaji kutoka kwa jamii ya kimataifa kuwa inatumia njaa kama silaha ya vita katika eneo hilo, kwani bado mashirika ya kutoa usaidizi yanasema yanapata shida kufika katika maeneo mengine.

Marekani imewawekea vikwazo baadhi ya maafisa wa serikali ya Ethiopia kutokana na jukumuj lao kwenye vita hivi ambavyo vimekuwepo tangu mwezi Novemba mwaka uliopita. Kwa kila hali, vita hivi vimempunguzia Waziri Mkuu Abiy Ahmed, mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel, uungwaji mkono wa ndani na wa kimatafa.

Mbali na vita vya Tigray, uchaguzi mwaka huu unafanyika huku uchumi unaendelea kukumbwa na changamoto. Bei ya bidhaa imeendelea kupanda, thamani ya sarafu ya Biir inaendelea kushuka mbele ya dola, na huku wawekezaji wengi wamerejesha nyuma nia yao ya kuwekeza humu nchini, na wale ambao tayari wamepiga kambi hapa wanapunguza fedha ambazo wanaweka katika uzalishaji.

Vile vile mapigano ya kikabila yamefanya maeneo kadhaa kushindwa kufanya shughuli zozote za kimaendeleo. Mbali na kaskazini mwa nchi, maeneo mengine kama magharibu na kusini mwa nchi yanaendelea kuripoti vita kwa maeneo kadhaa.

Uchaguzi wa mwaka huu pia unafanyika huku baadhi ya waliokuwa na nia ya kugombea wako jela, kwa mashitaka ya kufanya vurugu katika maneneo kadhaa nchini. Mmoja wa wagombea anawania wakati akiwa jela.

Kuna vyama ambavyo vimejitoa kwenye uchaguzi wenyewe vikidai kuwa havina uhuru.

Hata hivyo, waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa wakiwemo wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika wameshaanza kuwasili.

Waliojiandikisha nao wanangoja Jumatatu kwenda kuwasilisha matakwa yao kupitia kura yao.