Estonia yaongeza vikwazo dhidi ya viongozi wa Georgia
16 Desemba 2024Nchi hiyo imesema hatua hiyo ni jibu kwa ukandamizaji uliofanywa na watawala wa Georgia dhidi ya maandamano ya kuunga mkono mahusiano ya karibu na Umoja wa Ulaya.
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Estonia imesema vikwazo hivyo vya nyongeza vinawahusu maafisa 14 wanaobebeshwa dhima ya kuwakabili waandamanaji kwa mabavu. Miongoni mwao ni Waziri Mkuu wa Georgia, Irakli Kobakhidze, ambaye yeye na wenzake 13 watazuiwa kuingia Estonia.
Waziri wa Mambo ya Kigeni wa Estonia, Margus Tsahkna, amesema nguvu ambazo mamlaka za Georgia zinatumia "kuwakabili waandamanaji, waandishi habari na viongozi wa upinzani hazikubaliki."
Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Estonia pia ametoa rai kwa nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Ulaya kuchukua hatua nzito dhidi ya wote wanaotumia nguvu kupita kiasi kuzima maandamano ya Georgia.
Maandamano yalizusha nchini Georgia mnamo mwezi Oktoba baada ya Waziri Mkuu Kobakhidze kutangaza uamuzi wa kuchelewesha mazungumzo ya nchi yake kujiunga na Umoja wa Ulaya.