1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Dunia yaadhimisha uhuru wa vyombo vya habari

3 Mei 2021

Tarehe 3.5 kila mwaka dunia inaadhimisha uhuru wa vyombo vya habari, huku kaulimbiu ya mwaka huu ikisema ''Habari kwa Faida ya Umma''. Kaulimbiu hii inasisitiza umuhimu wa habari iliyothibitishwa na ya kuaminika.

https://p.dw.com/p/3su5o
Deutschland Symbolbild Pressefreiheit
Picha: Imago Images/S. Boness

Kaulimbiu hii inasisitiza umuhimu usiopingika wa habari iliyothibitishwa na ya kuaminika. Inatoa wito wa kuzingatia jukumu muhimu la waandishi habari kuwa huru na kufanya kazi kwa weledi katika kutoa na kusambaza habari.

Katika kuadhimisha siku hii DW imetoa Tuzo ya Uhuru wa Kujieleza kwa mwandishi wa Nigeria, Tobore Ovuorie mwandishi wa habari za uchunguzi. Ovuorie amekuwa akipigania kupaza sauti kwa jamii ya wasiosika nchini Nigeria. Ujasiri wake karibu uyagharimu maisha yake kutokana na kuandika taarifa zinazohusu wahalifu wanaohusika na biashara haramu ya watu na biashara ya viungo vya binadamu.

Faharasi ya uhuru wa vyombo vya habari duniani 2021
Faharasi ya uhuru wa vyombo vya habari duniani 2021

Hali ya uhuru wa vyombo vya habari Afrika Mashariki-Tanzania

Serikali ya Tanzania imelaumiwa kwa kutoheshimu maamuzi ya mahakama yanatolewa kuhusu vyombo vya habari na wanahabari, huku hali hiyo ikitajwa kuwa ni ukandamizaji mkubwa wa uhuru wa vyombo vya habari unaofanywa kwa nguvu ya Dola. Katika maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari duniani ambayo hufanyika kila tarehe 3 mwezi Mei, wanahabari wameikumbusha serikali nchini humo kuyaangalia madhira yote yanayowakumba.

Katika kilele cha  maadhimisho hayo yaliyofanyika  katika ukumbi wa mikutano wa kimataifa AICC uliopo Arusha, waandishi wa habari wamesema kuna haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu uhuru wa vyombo vya habari na wanahabari nchini  Tanzania, kufuatia  hali ya usalama wao wawapo kazini kutoridhisha, huku wengine wakipigwa na kunyang'anywa vifaa vya kazi.

Waandishi wa habari pia wameeleza wasiwasi wao wa mamlaka za serikali kutoheshimu utawala wa sheria, baada ya kukaidi maamuzi ya mahakama ya kuvifungulia vyombo vya habari ambavyo vilifungiwa kufanya kazi zake.

Hata hivyo wizara ya habari nchini Tanzania imeendelea kusisitiza kwamba ipo pamoja na wanahabari na itaendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili, licha ya kutokuwa na jibu la moja kwa moja kuhusu kuyafungulia magazeti yaliyofungwa, usalama wa wanahabari na uhuru wa vyombo vya habari. Waziri wa habari nchini Tanzania Innocent Bashungwa amesema, wingi wa vyombo vya habari vilivyosajiliwa nchini Tanzania ni ishara ya wazi kwamba kuna uhuru wa vyombo vya habari.

Baadhi ya wanahabari waliohudhuria kilele cha maadhimisho hayo wanasema, wingi wa vyombo vya habari vilivyosajiliwa siyo ishara kwamba kuna uhuru wa habari, huku wakiwa na matumaini ya kupatikana kwa muafaka wa changamoto zinazowakabili. 

Waandishi wa habari wa Misri wakishiriki maandamano mwaka 2016
Waandishi wa habari wa Misri wakishiriki maandamano mwaka 2016Picha: Amr Sayed/Apa/Zuma/picture alliance

Pamoja na hayo lakini pia wanahabari wameipongeza serikali hasa hii ya awamu ya sita kwa hatua zinazotia matumaini ya kuanza kushughulikiwa kwa changamoto za kihabari zinazoikabilia tasnia hiyo nchini Tanzania. 

Kenya

Huku ulimwengu ukiadhimisha siku ya uhuru wa vyombo vya habari, nchini Kenya wanahabari wanakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kukosa malipo yanayokidhi na pia unywanyasaji wa kingono dhidi ya wanahabari wa kike.

Mkuu wa mipango katika baraza la vyombo vya habari nchini Kenya, Victor Bwire anaeleza kwamba wanahabri habari nchini Kenya wanatimiza majukumu yao ya kufichua habari mbali mbali za kuwajibisha serikali na taasisi mbali mbali lakini wanakosa hata fedha za kwenda nyanjani kutafuta habari.

Warda Ahmed ni mwanahabari katika kituo cha redio cha Sauti ya Pwani nchini Kenya ameeleza kwamba wanahabari wengi walio na vipawa wanaingilia kazi nyengine kwa kukosa fursa za ajira na pia baadhi ya viongozi wa kiserikali bado hawawathamini kama wadau muhimu.

Ripoti ya baraza la wanahabari wa Afrika inaeleza kwamba miaka zaidi ya 30 sasa tangu kupitishwa kwa azimio la uhuru wa vyombo vya habari katika kongamano la Windhoek nchini Nambia bado wanahabri wanakosa usalama. Mwenyekiti wa chama cha wanahabari nchini Kenya Oloo Janak amezitaka serikali mbali mbali kushirikiana na wanahabari na pia kuwapa usalama wa kutosha.

Waandishi: Veronica Natalis, Faiz Musa