Tanzania: Hofu ya matukio ya utekaji nyara yaongezeka
30 Agosti 2024Wakati dunia ikiwa kwenye kumbukumbu Watu Waliotoweka, hapa Tanzania pamekuwa na mfululizo wa matukio ya watu kupotea au kutoweka katika mazingira ya kutatanisha, hali ambayo mara kadhaa imewaibua wanasiasa wanaoitupia lawama serikali kuhusika na upoteaji huo.
Baadhi ya matukio ya watu kupotea, ni pamoja na lile la Juni mwaka huu ambapo , Edgar Mwakalebela maarufu Sativa, mkaazi wa Dar es Salaam na mraghabishi wa mitandao ya kijamii, alitoweka nyumbani kwake, na baadaye alipatikana akiwa amejeruhiwa huko mkoani Katavi, mbali kabisa na Dar es Salaam.
Kadhalika Mwenyekiti wa Baraza la Vijana la Chadema kanda ya Temeke, Deusdedith Soka, naye anadaiwa kutoweka tangu Agosti 18 mwaka huu na mpaka sasa hajapatikana.
Soma pia:Tanzania: mtoto mwenye ualbino atoweka
Matukio mengine yanayofanana na hayo ni ya kupotea kwa watoto ambapo mtoto Angel John mkaazi wa Kibaha alipotea mnamo Mei 6 mwaka huu na baadaye mwili wake ulikutwa akiwa tayari ameshafariki.
Kadhalika lipo tukio la Mkaazi wa Mbweni jijini Dar es Salaam, Mohamed Ali Jabiri, ambaye alitoweka na siku kadhaa baadaye mwili wake ulipatikana akiwa ametobolewa macho.
Raia wataka matukio hayo kukomeshwa
Ukiachilia matukio hayo, Agosti Mosi mwaka huu wakaazi wa mkoa wa Simiyu waliandamana wakishinikiza serikali kuwapa majibu juu ya matukio ya watoto kupotea.
Wachambuzi wa mambo wanasema, matukio haya hayapaswi kubebwa kisiasa, na badala yake kunapaswa kufanyika mdahalo wa kitaifa kuyazungumzia.
Akizungumza bungeni Februari mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mohamed Masauni alitoa ufafanuzi wa matukio ya watu kutekwa na akasema, kuanzia Januari hadi Desemba 2023, akisema asilimia 72 ya waliopotea walikuwa wamepatikanana kisha akaongeza kuwa, sababu za watu kupotea ni pamoja na imani za kishirikiana, wivu wa mapenzi, visasi na ama kile alichokiita "kujiteka."
Soma pia:UN:Korea Kaskazini imehusika kutekwa kwa watu
Hata hivyo, Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika, (TLS) Boniphaxe Anyisile Mwabukusi,mara kadhaa wamekemea matukio hayo.
Siku ya Kimataifa ya watu Walitoweka huadhimishwa kila ifikapo Agosti 30 kama sehemu ya kukumbushana kuhusu hatma ya ndugu, marafiki na wenzetu waliopotea, katika mazingira ya kutatanisha na hali za migogoro kama vita na uhalifu.