Dkt Habineza: Kagame kabidhi madaraka, fuata katiba
14 Julai 2022Dkt Habineza kutoka chama pinzani cha Demokrasia na Ustawi wa Mazingira nchini Rwanda, ambaye pia ndiye muasisi,anasema Rwanda inahitaji makabidhiano ya madaraka kwa amani na rais Kagame hatakiwi kufanya kama walivyofanya watangulizi wake ambao baadhi waliuawa huku wengine wakitupwa jela.
Katika mahojiano na televisheni ya France 24 mapema wiki hii, Rais Kagame alisema ataiongoza Rwanda kwa miaka 20 ijayo endapo Wanyarwanda wataamua iwe hivyo.
Soma Pia:Kongo yaishutumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23
"Nitagombea urais kwa miaka 20 ijayo, sioni tatizo, uchaguzi ni suala la watu kuamua, si ndiyo?" Alisema rais Kagame.
"Tumelaumiwa kwa vitu vingi lakini hakuna aliyesema uchaguzi wetu haujawa wa haki na huru kama ilivyo kwa nchi zingine zikiwemo zile za watu wanaotulaumu" Aliongeza katika maelezo yake.
Kauli ya Kagame yazua mjadala mpana
Rais wa chama cha upinzani cha Demokrasia na Ustawi wa Jamii ambaye pia ni mbunge, Dkt Frank Habineza, amesema ameshangazwa na kauli hiyo.
Ameiambia DW kwamba kauli ya rais Kagame imetikisa siasa za Rwanda kwa sababu haina nia njema katika kuheshimu katiba ya taifa hilo la ukanda wa maziwa makuu.
"Kauli yake ilikuwa ni ya kushtusha kwa sababu inakwenda kinyume na katiba maana katiba inamruhusu kuongoza hadi mwaka 2034"
Alisema na kuongeza kwamba, kwa mantiki hiyo Kagame ataliingiza taifa katika mchakato wa kubadili katiba kama ilivyofanyika mwaka 2015.
Dkr Habineza alisema endapo kutakuwa na mpango wa kubadilisha katiba, chama chake kitasimama imara kupinga mpango huo katika Mahakama Kuu.
Anasema ingawa raia walionekana wakiomba katiba ibadilishwe mwaka 2015, lakini haikuwa kwa nia yao bali waliagizwa kufanya hivyo na viongozi wao.
Soma Pia:Viongozi wa DR Congo na Rwanda kufanya mazungumzo nchini Angola
Mbunge huyu anasema chama chake kinamtaka Rais Kagame aheshimu katiba ili hatimaye asijikute anaondoka mamalakani kwa namna ambayo itadhalilisha hadhi yake kama kiongozi kama ilivyotokea kwa watangulizi wake.
Habineza: Kagame kabidhi madaraka kwa mujibu wa katiba
Mwanansiasa huyo ambae amekuwa wakwanza kujitokeza hadharani na kulaani kauli hiyo ya rais Kagame ilionesha nia ya kuendelea na madaraka amesema wanataka kuona Rwanda inakuwa na utamaduni wa kukabidhi madaraka kwa amani.
Akimulika baadhi ya mataifa ambayo kwa kiwango kikubwa yamejikuta yakitumbukia katika mgogoro wa kisiasa na kusababisha machafuko amesema taifa lake halijabahatika bado viongozi wa juu kukabidhi madaraka kwa amani.
Soma Pia:Human Rights Watch yalaani ukandamizaji nchini Rwanda
"Rais wa awamu ya kwanza Kayibanda alifia jela, Habyarimana alikufa kwa kudunguliwa ndege aliyokuwemo, Bizimungu alitupwa jela, tunaomba Rais Kagame atupe zawadi aondoe huo mkosi"
Aliiambia Dw katika mahojiano maalum kufuatiarais Kagame kuonesha nia ya nwazi kuendelea na muhula mwingine wa uongozi licha ya katiba ya taifa hilo kumuweka kando.
"Kama ataachia madaraka kwa amani atakuwa ameandika historia mpya.” Alisisitiza
Dkt Habineza aliwania urais mwaka 2017 akashindwa, na safari hii chama chake kimeshamtangaza kuwa ndiye kitamsimamisha kukiwakilisha katika uchaguzi ujao wa mwaka 2024.