1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kifungo cha miaka 15 jela kwa mkosoaji wa Kagame

1 Oktoba 2021

Mkosoaji wa utawala wa Rais Paul Kagame aliyejizolea umaarufu mkubwa kutokana na video zake kupitia mtandao wa Youtube amehukumiwa miaka 15 jela mjini Kigali.

https://p.dw.com/p/418BS
Ruanda 25. Jahrestag Völkermord | Zeremonie in Kigali | Gefangene
Picha: Getty Images/A. Renneisen

 

Yvonne Idamange mwenye umri wa miaka 42 na mama wa watoto 4, hakuwepo katika korti hiyo mjini Kigali wakati hukumu hiyo ikitolewa. Amekutwa na makosa sita ikiwa ni pamoja na uchochezi wa ghasia na uasi, kupuuza kumbukumbu za mauaji ya kimbari, kueneza habari za uzushi na kuchochea vurugu.

Alishtumiwa kwa kuwa, katika mtandao wake wa Youtube, Bi Idamange alimshtumu Rais Kagame na serikali yake kwa kuanzisha udikteta, kutumia mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 kwa maslahi yao bila ya kuwapa msaada wowote wahanga na kugeuza eneo la kumbukumbu za mauaji hayo ya kimbari kuwa vivutio vya utalii.

Bi Idamange ambae mtandao wake wa youtube una wafuasi 18,900 na ambae video zake huangaliwa kwa wastani mara laki moja, anajinasibu kama mhanga wa mauaji ya kimbari ya Rwanda ambayo kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, yalisababisha vifo vya watu zaidi ya laki nane, wengi wao wakiwa kutoka jamii ya walio wachache ya Watutsi. Alishtumiwa pia kwa kumpiga na kumjeruhi afisa wa polisi wakati wa kukamatwa kwake.

Mbali na kifungo cha miaka 15 jela, alipigwa faini ya kiasi cha dola za kimarekani 2000. Awali,upande wa mashtaka ulipendekeza miaka 30 jela na faini ya dola 6000. Idamange amekua akisusia vikao vya mahakama hiyo ambayo alisema ni ya upendeleo, baada ya ombi lake la kutaka kesi yake ipeperushwe moja kwa moja mitandaoni kukataliwa.

Vitendo hivi vimekua vikiongezeka nchini Rwanda

Kizito Mihigo
Muimbaji na Mwanaharakati wa Rwanda Kizito Mihigo akiondoka katika gereza la Nyarugenge mwaka 2018.Picha: Getty Images/C. Ndegeya

Shirika la kimataifa la kutetea haki za binaadamu la Human Right Watch, lilizungumzia wasiwasi wake mwezi machi juu ya kuongezeka kwa vitendo vya kukamatwa na kushtakiwa kwa watu wanaokosoa mamlaka za Rwanda kwenye mitandao.

Shirika hilo lilikumbusha kauli ya vitisho ya Rais Kagame ya mwaka 2019, aliposema na hapa namnukuu:" Wale mnaowasikia wakizungumza mitandaoni, wapo Marekani, Afrika ya Kusini au Ufaransa. Kwa sababu wapo mbali, Wanafkiri wapo kwenye usalama. Lakini wapo karibu na moto, na siku watakapoukaribia, basi moto utawaunguza."mwisho wa kumnukuu rais Kagame

Rwanda inayotawaliwa kwa mkono wa chuma na rais Paul Kagame tangu kumalizika kwa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, hukosolewa mara kwa mara kwa kuwakandamiza wapinzani na kuuminya uhuru wa kujieleza.