1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Corona: Nchi za Ulaya zapambana kuzuia maambukizi mapya

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel
11 Machi 2020

Nchi za Ulaya zinafanya kila jitihada kuzuia kusambaa zaidi virusi vya corona kutoka nchini Italia. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuweka marufuku ya safari na kuongeza hatua za tahadhari.

https://p.dw.com/p/3ZCeY
Brüssel | Pressekonferenz Ursula von der Leyen und Charles Michel nach Treffen mit Erdogan
Picha: Getty Images/AFP/J. Thys

Jumuiya ya umoja wa Ulaya imesema itafanya kila lililo muhimu  kuanzia kuruhusu misaada ya serikali kwa makampuni, kuanzisha mfuko wa uwekezaji wa thamani ya euro bilioni 25 ili kukabiliana na kuporomoka kwa uchumi kutokana na mlipuko wa virusi cya COVID 19. Viongozi wa jumuiya hiyo walitangaza maamuzi hayo Jumanne 10.03.2020 baada ya kumalizika mkutano wao walioufanya kwa njia ya video.

Rais wa Halmashauri ya Ulaya Charles Michel amezisihi nchi wanachama kushirikiana katika kupambana na mlipuko wa virusi vya Corona ambavyo vitatishia kusababisha mgogoro wa kiuchumi. Akizungumza katika mkutano huo Rais wa Tume ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema tume hiyo itaandaa mpango wa kukabiliana na virusi vya  corona kwa kuwekeza fedha za kusaidia nchi wanachama endapo zitakabiliwa na matatizo ya kiuchumi kutokana na kuendelea kuenea kwa virusi vya corona.

Baadhi ya raia wa China waliotibiwa na kupona kutokana na kuambukizwa virusi vya corona watoka hospitali mjini Wuhan.
Baadhi ya raia wa China waliotibiwa na kupona kutokana na kuambukizwa virusi vya corona watoka hospitali mjini Wuhan.Picha: picture-alliance/Photoshot/Chen Yehua

China imesema abiria wote kutoka nchi za nje wanaofika mjini Beijing ni lazima wawekwe karantini kwa muda wa wiki mbili ili kuzuia maambukizi mapya. China ilikuwa tayari imeweka tahadhari kwa wageni wanaoingia nchini humo kutoka Korea Kusini, Iran, Italia na Japan.

Nchini Italia zaidi ya watu 10,000 wameambukizwa virusi vya corona huku idadi ya vifo ikiongezeka nchini humo wengi wao wakiwa ni wazee. Nchini Marekani maambukizi yameongezeka, zaidi ya watu 1000 wameambukizwa. Korea Kusini, imeripoti idadi ya maambukizi mapya hadi kufikia leo ni 242.

Thailand imesema haitotoa tena visa kwa wageni kutoka nchi zote ambao hapo awali walistahili kupewa visa mara baada ya kuingia nchini humo na badala yake wageni wote wanatakiwa kuomba visa kwenye balozi zake kabla ya kusafiri. Australia imetangaza kuuongeza fedha mfuko wa afya kwa takriban dola bilioni 2.4 ambazo zitatumiwa kuanzisha kliniki za homa, pamoja na hatua zingine za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.

Vyanzo: /DPA/AFP/RTRE