COP15: Je, bioanuwai ni nini hasa?
7 Desemba 2022Bioanuwai inamaanisha anuwai jumla ya kibayolojia na kijeni ya viumbe hai na mifumo ya ikolojia kwenye sayari yetu. Viumbe hai vinajumlisha mamalia na mimea na pia kuvu na vijidudu wadogo wanaopatikana kwenye udongo. Mifumo mbalimbali ya ikolojia ni tofauti kama vile Antarctic, misitu ya mvua ya kitropiki, Sahara, misitu ya mikoko, pori la beech nyekundu wa Ulaya ya Kati au maeneo mbalimbali ya baharini na pwani duniani kote.
Soma pia: Mkutano wa Bayoanuwai COP15 wafunguliwa Canada
Makazi hayo yanatupatia sisi wanadamu idadi kubwa ya vitu tunavyohitaji kuishi, kama vile maji, chakula, hewa safi au dawa. Mifumo ya ikolojia hivyo hutoa kile kinachoitwa huduma za mfumo wa ikolojia - na hizi pia zinategemea mwingiliano wa spishi anuwai. Ikiwa sehemu moja moja zitaanguka, kwa mfano kwa sababu spishi zitatoweka, katika hali mbaya zaidi huduma hizi zinazotolewa na asili kwa ajili yetu pia hupotea.
Kwa maneno mengine: Bila mwani au miti hakuna oksijeni. Bila wadudu wa kuchavusha mimea, tusingeweza kuvuna chochote. Kwa sababu zaidi ya theluthi mbili ya mazao yote, ikiwemo aina nyingi za matunda na mboga, kahawa na kakao, hutegemea uchavushaji wa asili kama vile wadudu. Lakini theluthi moja ya spishi zote za wadudu ulimwenguni tayari ziko kwenye hatari ya kutoweka.
Soma: Mazungumzo ya kupambana na upotezaji wa bioanuwai yaanza China
Jinsi maisha yetu yanavyotegemea huduma za asili
Ingawa hatuwezi kuishi bila huduma hizi zinazotolewa na maumbile ya asili, mara nyingi tunazichukulia kawaida, anasema Dave Hole. Mtaalamu huyo wa jenetiki ya ikolojia ameandika utafiti mpya pamoja na wengine kwa shirika la mazingira la Conservation International, ambalo linaangazia huduma za mfumo wa ikolojia.
Kulingana na utafiti huo, hadi asilimia 70 ya mavuno ya dunia yanategemea moja kwa moja au kwa njia zisizo za moja kwa moja kuta za vizuwizi na miti shamba, miongoni mwa mambo mengine kwa sababu hulinda maeneo ya kulima mazao ya chakula kutokana na mafuriko. "Tunapokula bakuli la muesli asubuhi, kwa ujumla hatufikirii sana juu ya kile asili imefanya ili kutuwezesha kula muesli hii," Hole alisema katika mahojiano ya DW.
Soma pia:Umoja wa Mataifa kufanya mkutano wa kwanza kuhusu mzozo wa Bioanuwai
Kamati ya kiserikali ya Umoja wa Mataifa kuhusu Anuwai za Kibayolojia (IPBES) inakadiria kuwa kuna angalau spishi milioni 8, lakini kufikia 2030 hadi milioni moja zinaweza kutoweka milele. Tayari, upotevu wa bayoanuwai umefikia kiwango kikubwa zaidi - sawa na spishi moja inayokufa kila dakika kumi. Kulingana na sayansi, tuko katikati ya kutoweka kwa spishi kwa sita ulimwenguni.
Nchini Ujerumani pekee, idadi ya wadudu wanaoruka ilipungua kwa robo tatu kati ya 2008 na 2017. Idadi ya wanyama pori ilipungua kwa asilimia 82 duniani kote, kulingana na IPBES. Idadi ya wanyama na aina za mimea wanaoishi katika maji yasiyo na chumvi imepungua duniani kote kwa asilimia 83 katika miaka 50 iliyopita, na katika Amerika ya Kati na Kusini ilikuwa asilimia 94 ya viumbe hao, kulingana na utafiti wa shirika la mazingira WWF.
Na kulingana na Hole, upotezaji wa anuwai ya kibayolojia hufanyika kwa kasi kubwa - kasi inaongezeka hata.
Wanadamu wanahusika na kutoweka kwa viumbe
Sayansi inakubali: kwa sababu ya kilimo, ufunikaji wa ardhi, usafishaji misitu, uvuvi wa kupita kiasi, kuenea kwa viumbe vamizi na wanadamu, kiwango cha kutoweka leo ni hadi mara 100 zaidi kuliko inavyokuwa pasina ushawishi wa binadamu.
Elizabeth Maruma Mrema, Katibu Mtendaji wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa wa Anuwai ya Bayolojia (CBD), ameweka wazi kabisa katika mazungumzo na DW, akisema shughuli za binadamu zimesababisha uharibifu wa asilimia 97 ya viumbe hai duniani.
Takwimu zilizoorodheshwa na mkuu wa CBD ni za kutisha. Kulingana na takwimu hizo, asilimia 75 ya eneo la ardhi kwa sasa limeharibiwa na asilimia 66 ya bahari, asilimia 58 ya nyanda zote za ardhi yowevu zinatishiwa au tayari zimetoweka na nusu ya miamba ya matumbawe tayari imekufa. Mrema anasisitiza kuwa takwimu hizo hazizingatii hata uchafuzi wa sayari kwa taka za plastiki.
Upotevu wa viumbe hai unatishia sayari na ubinadamu
"Upotevu unaoendelea wa mtaji wetu wa asili unaleta tishio kubwa zaidi kwa wanadamu wote," anaonya Klement Tockner, Mkurugenzi Mkuu wa Jumuiya ya Senckenberg ya Ujerumani na Profesa wa Sayansi ya Mfumo wa Ikolojia. "Kwa sababu inapopotea, imepotea milele."
Soma pia: WWF: Kuna kitisho kikubwa kwa viumbehai na bioanuwai duniani
Pale spishi zinapotoweka kwenye mfumo wa ikolojia, hauporomoki kabisa, lakini unabadilika. "Kadiri tunavyopunguza spishi, ndivyo mfumo unavyoathiriwa zaidi," anaelezea Andrea Perino kutoka Kituo cha Utafiti wa Bioanuwai cha Ujerumani (iDiv) katika Chuo Kikuu cha Halle-Jena-Leipzig.
Kama ilivyo kwa hali ya hewa, pia kuna kile kinachoitwa vidokezo katika mifumo ya ikolojia ambapo matukio yanaweza kutokea na kusababisha hatua zisizoweza kuzuilika, anasema Dave Hole. Mfano wa hii ni msitu wa mvua katika eneo la Amazon. Baada ya msitu huo kufyekwa sana, sehemu iliyobaki pia inazidi kuwa mbaya na mbaya zaidi. Na hiyo inaongeza hatari kwamba msitu wote wa mvua utakufa.
Misitu ya kitropiki kama Amazon ni makazi ya karibu theluthi mbili ya viumbe vyote vinavyojulikana duniani kote, na ni muhimu sana kwa tabianchi ya dunia.
Tunahitaji kuilinda vyema asili - kwa maslahi yetu wenyewe
Bila hatua kubwa za kuzuia kupotea kwa bayoanuwai, msingi wa asili wa maisha ya binadamu utapotea kwa kasi isiyokuwa ya kawaida - na madhara ya muda mrefu kwa karibu nyanja zote za maisha.
Asilimia 50 ya uzalishaji wa uchumi wa dunia unategemea moja kwa moja asili, anasema Katibu Mtendaji wa CBD Mrema. "Tunaharibu asili ingawa mapato yetu, chakula chetu, afya zetu na hewa tunayovuta vinaitegemea."
Mwandishi: Jeannette Cwienk