Congress yathibitisha ushindi wa Trump
7 Januari 2025Kinyume na hali ilivyokuwa miaka minne iliyopita, siku ya Jumatatu (Januari 6) bunge la Marekani lilifanikisha kwa wepesi tukio hilo ambalo ni alama ya mila ya kidemokrasia kwa taifa hilo kubwa duniani bila ya mashaka yoyote.
Makamu wa Rais Kamala Harris alisimamia zoezi hilo la kuhisabiwa kura za wajumbe na kisha akamtangaza rasmi aliyekuwa mpinzani wake kwenye uchaguzi wa Novemba 9 kuwa ndiye mshindi halali.
Soma zaidi: Waziri Mkuu wa Italia afanya ziara ya kushtukiza kwa Trump
"Matokeo ya kura ya rais wa Marekani, kama yalivyowasilishwa kwa rais wa Baraza la Seneti ni kama ifuatavyo. Idadi kamili ya wajumbe walioteuliwa kumchagua rais wa Marekani ni 538. Ndani yake, wingi wa kura ni 270. Kura za rais ni kama ifuatavyo: Donald J. Trump wa jimbo la Florida amepata kura 312. Kamala D. Harris wa jimbo la Carlifornia amepata kura 226. Kura za makamu wa rais ni kama ifuatavyo: J.D. Vance wa jimbo la Ohio amepata kura 312. Tim Walz wa jimbo la Minnesota amepata kura 226." Alisema makamu huyo wa rais.
Kabla ya kutoa tangazo hilo, Kamala Harris alikuwa ametekeleza wajibu wake huo wa kikatiba kwa kusimama kwenye ukumbi wa bunge akipitisha kila nakala ya matokeo ya uchaguzi kwa wabunge na kila karatasi ya matokeo ya kura ilipotajwa alisimama akiwa amekunja mikono yake.
Baadaye, makamu huyo wa rais kutokea chama cha Democrat aliwaambia waandishi wa habari kuwa kwake ilikuwa siku muhimu muhimu sana kwa demokrasia ya Marekani, akiongeza kwamba "hii ndiyo mila Wamarekani wanayopaswa kuifurahikia, ambayo ni mojawapo wa misingi muhimu ya demokrasia yetu, yaani kuwa ni ukabidhianaji wa madaraka kwa njia za amani. Na leo nimetenda kile ambacho nimekuwa nikikifanya maishani mwangu mote, ambacho ni kutimiza kiapo changu cha kuilinda katiba ya Marekani."
Kamala aingia kwenye historia
Kwa kitendo hiki, Kamala Harris alikuwa anajiunga na orodha ya watangulizi wake ambao walisimamia shughuli ya kuthibitisha kushindwa kwao kwenye uchaguzi kama sehemu ya majukumu yao ya kikatiba kwenye bunge.
Richard Nixon alifanya hivyo hivyo pale aliposhindwa na John F. Kennedy mwaka 1960 na akafuatiwa na mgombea urais kwa tiketi ya Democrat mwaka 2000, Al Gor, pale Mahakama ya Juu ya Katiba iliporidhia kuchaguliwa kwa George W. Bush.
Soma zaidi: Trump kuhukumiwa katika kesi ya hongo kabla ya kuapishwa
Lakini haijawahi kutokea makamu wa rais aliyepigania uchaguzi wa rais kusimamia kuthibitisha matokeo ya rais ajaye ambaye mwenyewe aliwahi kukataa kushindwa kwenye uchaguzi uliopita.
Mnamo tarehe 6 Januari 2021, wafuasi wa Donald Trump, aliyekuwa wakati huo ameshindwa kwenye uchaguzi wa rais na Joe Biden, walilivamia jengo la Capitol Hill, na kusababisha madhara makubwa yakiwemo vifo, katika jaribio la kulizuwia bunge kumuidhinisha rasmi Joe Biden.
Hadi sasa, watuhumiwa wa machafuko hayo wanaendelea kushikiliwa jela, na wengi wanatazamia watatangaziwa msamaha mara tu Trump atakapoapishwa wiki mbili zijazo.