Christine Lagarde aisifu Kenya
7 Januari 2014Hayo ni kwa mujibu wa Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Fedha duniani Bi Christine Legarde ambaye yuko katika ziara rasmi ya siku tatu nchini Kenya. Lagarde ambaye alifanya mazungumzo na rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta siku ya Jumatatu aliipongeza nchi hiyo.
“Nchi yako imekuwa kielelezo kwa kukamilisha mpango wa maendeleo kupitia mkopo ulioanza miaka mitatu iliyopia. Imekuwa pia kielelezo kwa kupata Katiba mpya mwaka 2010 na kuleta mageuzi kwa ajili ya ukuaji wa uchumi na Kenya imekuwa kielelezo kwa Afrika Mashariki”.
Umuhimu wa kuimarisha uchumi
Lagerde aliyewasili mjini Nairobi siku ya Jumatatu alifanya mashauriano na waziri wa fedha Henry Rotich kabla kukutana na rais Uhuru Kenyatta. Rais Uhuru Kenyatta kwa upande wake amesema serikali yake inatambua umuhimu kuimarisha ukuaji wa uchumi na ndio maana ifanya kila iwezalo kubuni nafasi za kazi na kupunguza umasikini.
“Tunafanya hivi kwa kuhakikisha uchumi wetu unakua kupitia uwekezaji katika miundo mbinu kuhakikisha ushirikiano wa kimataifa ya eneo hili. Tunaangazia upanuzi wa mifumo ya usafiri kupanua uzalishaji wa nguvu za umeme pamoja na kujenga reli za kisasa na bandari ili kukukuza uchumi wetu na kubuni nafasi za kazi na kukuza uchumi wetu”
Mapambano dhidi ya ufisadi
Uhuru alimhakikisha mkurugenzi huyo wa shirika la fedha duniani kwamba serikali yake inapiga vita ufiisadi ili Kenya iweze kushindana kikamilifu katika uchumi wa ulimwengu. Kenya mwezi huu inakamilisha mpango wa ustawi wa kiuchumi wa miaka mitatu uliofadhiliwa na shirika hilo la fedha kwa kiasi cha shilingi bilioni 65 ambazo ni sawa na sawa na dola milioni 750.
Lengo kuu la mkopo huo lilikuwa kuisaidia Kenya kukabiliana na changamoto za kiuchumi za ndani na nje ya nchi ambazo zimeyumbisha uchumi tangu mwaka 2011. Miongoni mwa changamoto hizo ni ugaidi, ukosefu wa usalama, ufisadi na kudorora kwa miundo mbinu.
Bi Cristine Lagerde aliipongeza Kenya kwa kujikwamua kiuchumi licha ya changamoto hizo na kuahidi kuendeleza uhusiano kati ya shirika lake na Kenya. “Tumefurahi kuwa washirika na tutaendelea kuwa washirika ili kuwezesha nchi yako na uchumi wa nchi kuwa kielelezo,” alisema Lagarde.
Mkurugenzi huyo wa IMF yuko katika ziara ya mataifa ya kusini mwa Jangwa la Sahara na tayari ametembelea mataifa sita ikiwemo Côte d'Ivoire, Malawi, Niger, Nigeria, na Afrika Kusini.
Mwandishi: Alfred Kiti
Mhariri: Mohamed Khelef