China, Zambia, Tanzania zakubaliana kuikarabati TAZARA
4 Septemba 2024Mkataba huo umesainiwa wakati Rais wa China Xi Jinping akiwa ndiye mwenyeji wa mkutano wa tisa wa kilele kati ya China na Afrika unaoanza Jumatano.
Rais Xi Jinping ameshuhudia utiwaji saini wa makubaliano ya ukarabati wa reli ya Tanzania na Zambia, TAZARA yenye urefu wa kilomita 1,860. Kulingana na shirika la habari la taifa la China la Xihua, mkataba huo ulitiwa saini na marais wa Zambia, Hakainde Hichilema na Tanzania, Samia Suluhu Hassan wanaohudhuria mkutano wa kilele wa ushirikiano kati ya Afrika na China.
Soma zaidi: Kongamano la China- Afrika kuja na matokeo yenye tija?
Reli ya TAZARA ilijengwa kati ya mwaka 1970 na 1975 kwa mkopo usio na riba kutoka China. Reli hiyo ni njia ya kusafirisha mizigo kutoka katika migodi ya madini ya shaba na kobalti ya Zambia hadi Tanzania. Ilianza shughuli zake mnamo mwaka 1976. Mradi huo wa miaka kadhaa ulihusisha ujenzi wa mamia ya madaraja na njia za chini ya ardhi zinazofanywa na maelfu ya wafanyakazi wa China na Afrika.
Mkutano wa kilele kufunguliwa na Xi Jinping
Huku hayo yakijiri Rais wa China Xi Jinping Jumatano atakuwa mwenyeji wa viongozi wa Afrika anakotarajiwa kuwashawishi viongozi wa bara hilo wanunue bidhaa nyingi zaidi kutoka nchini mwake kwa ahadi ya kuwapa misaada na uwekezaji zaidi. Viongozi 25 wa Afrika wameshawasili Beijing. China ambalo ni taifa la pili lenye uchumi mkubwa duniani ndiyo mshirika mkubwa wa kibiashara wa bara hilo.
Soma zaidi: Tanzania yatenga ardhi kwa Zambia kujenga bandari kavu
Mkutano huu wa tisa kati ya China na viongozi wa Afrika unatarajiwa kutoa muelekeo wa ushirikiano kati ya China na Afrika hasa baada ya kipindi cha janga la corona. Unafanyika wakati ambapo msuguano wa kisiasa unazidi kuongezeka katika ngazi ya kimataifa.
Katika mkutano huo, viongozi wa Afrika wanatafuta suluhisho la haraka la madeni yanayozidi kuongezeka barani humo, uwekezaji, na kuhakikishiwa kuwa miradi iliyoahidiwa katika mkutano wa mwaka 2021 wa Dakar itatekelezwa.
China, ambayo ni mkopeshaji mkubwa duniani inataka kupunguza kiwango chake cha uwekezaji mahali kwingine na kuboresha mahusiano yake na nchi zinazoendelea. Inataka pia kujikita katika kuwekeza kwenye miradi midogo midogo badala ya miradi mikubwa ya miundombinu.