China yaionya Korea Kusini kutoingiza siasa kwenye uchumi
26 Novemba 2023Waziri wa mambo ya nje wa China Wang Yi, amemuonya leo mwenzake wa Korea Kusini Park Jin kutoingiza siasa katika masuala ya uchumi na teknolojia. Wang ametoa matamshi hayo wakati mawaziri hao wawili wakijiandaa kukutana na mwanadiplomasia mkuu wa Japan Yōko Kamikawa, pembezoni mwa mkutano wa pande tatu unaolenga kuimarisha ushirikiano.
Kulingana na taarifa kutoka wizara ya mambo ya nje ya China, Wang amemueleza Jin kwamba China na Korea Kusini zimekuwa washirika wenye maslahi yanayofungamana pamoja na uzalishaji na usambazaji wa bidhaa.
Aidha waziri huyo wa China amesema kuwa pande zote mbili zinapaswa kuepusha kuingiza siasa katika masuala ya biashara.
Mawaziri hao watatu wa mambo ya nje wanakutana katika mji wa bandari wa Busan, katika mkutano wa kwanza kama huo tangu mwaka 2019. Mnamo Septemba, maafisa wakuu kutoka nchi hizo tatu walikubaliana kupanga mkutano wa kilele wa pande tatu haraka iwezekanavyo.