1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaSyria

Chanzo: Hezbolah imetuma wapiganaji 2000 nchini Syria

7 Desemba 2024

Chanzo cha karibu na kundi la wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon kimesema kwamba kundi hilo limewapeleka wapiganaji 2,000 nchini Syria karibu na maeneo ya mpaka wakati ambapo vikosi vya serikali ya nchi hiyo vikiondoka.

https://p.dw.com/p/4ns8R
Waasi wa Syria
Waasi nchini Syria wanaendelea kuchukua udhibiti katika miji nchini humoPicha: OMAR HAJ KADOUR/AFP/Getty Images

Chanzo cha karibu na kundi la wanamgambo wa Hezbollah wa Lebanon kimesema kwamba kundi hilo limewapeleka wapiganaji 2,000 nchini Syria karibu na maeneo ya mpaka wakati ambapo vikosi vya serikali ya nchi hiyo vikiondoka kutokana na mashambulizi ya waasi ambao wameiteka miji mikubwa katika siku za hivi karibuni.

Chanzo ambacho hakikutaka kuwekwa wazi kwa sababu za kiusalama kimeliambia shirika la habari la AFP kwamba kundi hilo limewapeleka wanajeshi hao katika eneo la Qusayr kwenda kulinda nafasi zake huko ingawa bado kundi hilo halikuwa limeshiriki vita vyoyote na waasi wa Syria.

Soma zaidi. Waasi Syria waitwaa Daraa

Kwa upande mwingine, duru zinasema wanajeshi wa Syria wameondoka katika maeneo yao katika jimbo la kusini la Quneitra linalopakana na Milima ya Golan inayokaliwa na Israel mapema hii leo.

Shirika linalofuatilia vita nchini Syria limeripoti kuwa serikali ya nchi hiyo imepoteza udhibiti wa jimbo na mji muhimu wa kusini, Daraa, ambao ndio chimbuko la vuguvugu la mwaka 2011 dhidi ya utawala wa Rais Bashar Assad. Hali ya kiusalama nchini Syria inatajwa kuwa inazidi kuwa mbaya na isiyotabirika.