1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Changamoto za kiusalama kuhusu uchaguzi Kenya

11 Mei 2022

Kenya inakabiliwa na hatari ya kuchagua asilimia 40 ya viongozi wahalifu au wafanyibiashara wa magendo kwenye uchaguzi mkuu ujao.

https://p.dw.com/p/4B9QQ
Kenia Wahlwiederholung |  Unabhängige Wahlkommission (IEBC)
Picha: Reuters/T. Mukoya

Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiangi ameelezea wasiwasi kwamba huenda viongozi wengi watakaochaguliwa kwenye uchaguzi mkuu ujao wakawa ni wahalifu wa kifedha, maarufu humu nchini kama ‘wash wash'.

Amesema wahalifu hawa wamepata mwanya wa kutumia pesa kujitafutia ushawishi wa umma, kufuatia mabadiliko kwenye sheria za fedha za kampeini za siasa na sheria za kukabiliana na makosa ya uchaguzi.

"Fedha zinazotumiwa na wasiasa kwa kampeini ni nyingi ajabu. Tutakuwa na matukio mengi kupita kiasi ya wapiga kura kuhongwa kwenye uchaguzi huu. Na siogopi kusema kwamba, tusipokuwa makini kama taifa, tutawachagua mamlakani viongozi ambao ni walanguzi wa dawa za kulevya na wahalifu wa viwango vya juu.”

Waziri huyo wa usalama wa ndani anaeleza kwamba kulingana na ripoti iliyo kwenye idara ya upelelezi, wanasiasa hao walio kwenye biashara za kihalifu wamekuwa wakiwakodisha watu na kuwasafirisha kwa mikutano ya umma ya kampeini za siasa kote nchini.Baadhi ya viongozi hawa wanaochunguzwa wana ushawishi mkubwa na wanaongoza kati ya wagombea viti kwenye maeneo yao.

''Mamlaka yetu sasa yameondolewa''

Waziri wa Kenya wa mambo ya nje Fred Matiangi
Waziri wa Kenya wa mambo ya nje Fred MatiangiPicha: Getty Images/AFP/S. Maina

Mwaka jana bunge la kitaifa lilifanya marekebisho kwenye sheria za uchaguzi na kuondoa vipengee vinavyodhibiti kiasi cha fedha kinachotumiwa na wanasiasa wakati wa uchaguzi. 

Kadhalika, mwenyekiti wa tume ya uchaguzi nchini IEBC, Wafula Chebukati, analalamika kwamba mahakama pia imekuwa ikitumiwa kuwaondolea mamlaka ya kushughulikia makosa ya uchaguzi.

"Tukilinganisha na mwaka 2017 ambapo tulifanikiwa kudhibiti joto la kisiasa, tukawazuia wanasiasa kutoharibu mabango ya wapinzani wao na kutodhulumiana kwenye maeneo ya kampeini za siasa, mamlaka yetu sasa yameondolowa.”

 Majukumu ya kisheria 

Hoja hizi zimezungumzwa kwenye kongamano la pili la mfumo wa haki wa makosa ya jinai lililofanyika kaunti ya Nakuru. Kongamano la kwanza lilifanyika mwaka 2019. Kongamano hili la siku tatu litaangazia mapambano dhidi ya ufisadi, namna haki inaweza kuwafikia waathiriwa kwa urahisi na kwa wakati unaofaa, kati ya mengineo. Jaji mkuu Martha Koome.

"Ni lazima tuangazie maswala yanayohimiza uwajibikaji. Hakuna mtu anapaswa kudhulumiwa kihaki kwa sababu tunashuhudia mchakato wa uchaguzi. Wakenya wamesubiri kwa hamu kusikia mikakati iliyowekwa ili kuhakikisha watu wamelindwa.”

Wadau hawa wanapendekeza kutungwa kwa sheria zitakazozuia viongozi wahalifu kuingia mamlakani.