Bola Tinubu mgombea wa chama tawala Nigeria
8 Juni 2022Rais Muhammadu Buhari anaachia ngazi mwakani baada ya kuliongoza taifa hilo lenye wakaazi wengi zaidi barani Afrika na msafirishaji mkuu wa mafuta kwa kipindi cha miaka minane kinachoruhusiwa kikatiba.
Tinubu mwenye umri wa miaka 70 alieliongoza jimbo la Lagos ambalo ndiyo mji mkuu wa kibiashara wa Nigeria kuanzia 1999 hadi 2007, amewashinda wagombea wengine 13, akiwemo naibu wa Buhari, makamu wa rais Yemi Osinbajo, katika mchakato wa kura za mchujo wa chama cha APC.
Mwanasiasa huyo anaejulikana kama baba wa ubatizo wa Lagos kutokana na ushawishi wake wa kisiasa, ameshinda kura 1,271 kati ya wajumbe 2,300 wa chama walioshiriki kwenye zoezi la upigaji kura, kulingana na matokeo yaliotangazwa na kituo kimoja cha televisheni nchini humo.
Soma pia: Wajumbe wa APC washiriki kura ya mchujo kumchagua mgombea urais
Wafuasi wa Tinubu wamelipuka kwa nderemo na vifijo huku wakiimba na kucheza katika uwanja wa Eagle ulioko mji mkuu wa Abuja, ambako zoezi la upigaji kura lilifanyika.
Tofauti na wakuu wengi wa kiafrika wanaomaliza muda wao, Rais Buhari hakuteua mrithi, na hivyo kuuacha wazi uwanja wa APC kwa wajumbe kuchagua mtu wamtakaye.
Mgombea wa chama tawala huchukuliwa kwa kawaida kuwa mwenye nafasi nzuri zaidi ya kushinda nchini Nigeria, ambayo ina historia ndefu ya udanganyifu wa uchaguzi na vurugu.
Hata hivyo mwaka 2015, Buhari alikuwa mgombea wa upinzani aliposhinda uchaguzi uliozingatiwa na wengi kuwa miongoni mwa chaguzi safi zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini humo.
Mbio za farasi wawili
Mpinzani mkuu wa Tinubu atakuwa Atiku Abubakar, ambaye aliwahi kuwa makamu wa rais kuanzia 1999 hadi 2007, chini ya rais wa zamani Olugegun Obasanjo. Atiku anagombea kwa tiketi ya chama cha People's Democratic Party, PDP.
Soma: Seneti Nigeria yabadili sheria ya matokeo ya uchaguzi
Tinubu ambaye anatajwa kuwa mwanasiasa mjanja, alijenga ngome imara ya wafuasi wakati wa kipindi chake cha miaka minane kama gavana wa Lagos.
Tangu alipoachia nafasi hiyo, alisalia kuwa mwenye ushawishi mkubwa, akiwa na wafuasi wengi watiifu katika nafasi zenye nguvu serikali na katika biashara.
Wafuasi wake wanamwelezea kama msimamizi mzuri na hodari wa kuchagua watendaji mahiri, waliojitolea kufanikisha kazi.
Soma pia: Maoni: Aliyeshinda na aliyeshindwa Nigeria wote wabaya
Wakosoaji wanamtuhumu kujichukulia kama mungumtu anaetoa kandarasi nono na ajira zenye malipo makubwa kwa marafiki zake, na hashindwi kuwatuma majambazi wa mitaani kuwatishia wapinzani iwapo anashindwa kufanikisha takwa lake.
Tibu hata hivyo anapinga kuelezwa hivyo.
Chanzo: Mashirika