Burundi yatangaza kufunga mpaka na Rwanda
12 Januari 2024Burundi ilitangaza jana kuufunga mpaka wake na Rwanda, wiki mbili baada ya kuituhumu nchi hiyo jirani yake kuunga mkono waasi waliofanya mashambulizi kwenye ardhi yake.
Waziri wa mambo ya ndani wa Burundi Matin Nitereste, aliwaambia waandishi habari hapo jana jioni kwamba wameamua kufunga mpaka na Rwandana kwamba yeyote anayejaribu kupitia mpaka huo hatofanikiwa.
Waziri Nitereste alisema Rwanda inawahifadhi wahalifu wanaowadhuru raia wa Burundi, na kuongeza kuwa wao pia hawawataki raia wa Rwanda. Burundi inasema kundi la waasi wa RED-Tabara walifanya shambulizi Desemba 22 karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuuwa watu 20, wakiwemo wanawake na watoto.
Tangu kutokea kwa shambulio hilo, Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amekuwa akiituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi hao, madai ambayo serikali ya Rwanda imeyakanusha mara kwa mara.