Burundi yafunga mpaka wake na Rwanda
11 Januari 2024Waziri wa Mambo ya Ndani wa Burundi Martin Niteretse amesema uamuzi huo umeafikiwa baada ya kubaini kuwa, Rwanda inawahifadhi wahalifu wanaowashambulia Warundi.
"Baada ya kubaini kuwa tulikuwa na jirani mbaya, Rais wa Rwanda Paul Kagame tulisitisha mahusiano naye hadi atakapobadilika kuwa bora," aliongeza waziri huyo.
Burundi inasema kundi la RED-Tabara lilifanya shambulizi Desemba 22 karibu na mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na kuua watu 20, wakiwemo wanawake na watoto.
Soma pia: Ndayishimiye aituhumu Rwanda kuwaunga mkono waasi wa Burundi
Rais Evariste Ndayishimiye wa Burundi tangu wakati huo amekuwa akiinyoshea kidole Kigali akiishtumu kuwaunga mkono waasi hao -- madai ambayo yamekanushwa na serikali ya Rwanda.
Uhusiano kati ya Burundi na Rwanda mara nyingi umekuwa na pandashuka chungumzima, ingawa ulianza kuimarika baada ya Ndayishimiye kuchukua madaraka mwaka wa 2020, lakini umedorora tena kutokana na ushiriki wa Burundi katika kampeni za usalama nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo
Kundi la RED-Tabara linashtumiwa kuendesha mashambulizi makali katika taifa hilo la Afrika Mashariki.Tangu 2015 kundi hilo halikuwa likifanya mashambulizi lakini tangu Septemba 2021, limekuwa likifanya mashambulizi kadhaa, ikiwa ni pamoja na dhidi ya uwanja wa ndege wa jiji kuu la Bujumbura.