Utawala wa kijeshi nchini Burkina Faso wazuia mapinduzi
28 Septemba 2023Taarifa ya utawala wa jeshi iliyosomwa kupitia kituo cha televisheni cha taifa imesema idara za usalama na ujasusi za Burkina Faso zimefanikiwa kuzuia jaribio la mapinduzi lililopangwa kufanyika Septemba 26.
Kulingana na taarifa hiyo, maafisa na watu wengine wanaodaiwa kuhusika na jaribio hilo lililonuia kuvuruga utulivu wamekamatwa na wengine bado wanasakwa.
Kiongozi wa kijeshi nchini humo Ibrahim Traore aliingia mamlakani Septemba 30, 2022, baada ya mapinduzi ya pili yaliyofanyika katika kipindi cha miezi minane.
Mapinduzi hayo, kwa sehemu yalichochewa na kutoridhishwa na hatua zinazochukuliwa katika kukomesha uasi wa jihadi nchini humo.
Jumanne usiku, maelfu ya watu waliingia katika mitaa ya mji mkuu Ouagadougou kufuatia mwito kutoka kwa wafuasi wa Traore wa "kumtetea" huku uvumi wa mapinduzi ukisambaa kwenye mitandao ya kijamii.
Taarifa ya utawala huo wa kijeshi aidha imesema "unasikitika kwamba maafisa ambao kiapo chao ni kutetea nchi yao wamepotoka na kuingia katika shughuli ya aina hii, ambayo inalenga kuzuia maandamano ya watu wa Burkinabe ya kutafuta uhuru na ukombozi kamili kutoka kwa makundi ya kigaidi yanayojaribu kuwafanya watumwa".
Taarifa zasema wanajeshi hao walikuwa wakichunguza makazi ya Traore na maafisa wengine
Mapema mwezi huu, mwendesha mashtaka wa utawala huo alisema wanajeshi watatu walikamatwa na kufunguliwa mashtaka ya kupanga njama dhidi ya utawala huo.
Soma pia: Wanajeshi wa Burkina Faso Na Mali wakutana kujadili usalama
Wachunguzi walidokezwa kwamba wanajeshi wa sasa na wa zamani waliofanyia idara ya ujasusi walikuwa wakiyachunguza makazi na maeneo mengine yanayotumiwa na watu muhimu katika utawala wa kijeshi, ikiwa ni pamoja na Traore mwenyewe.
Taarifa hiyo iliongeza kuwa walikuwa na lengo la "kuvuruga...mchakato wa mpito", ukirejelea neno linalotumika kuelezea utawala wa kijeshi wa mpito kabla ya uchaguzi ambao utawala huo umeahidi kwamba utafanyika.
Zaidi ya raia 17,000 na wanajeshi wamekufa katika mashambulizi ya jihadi nchini Burkina Faso, hii ikiwa ni kulingana na shirika lisilo la kiserikali la Armed Conflict Location and Event Data Project, ACLED.
Zaidi ya watu milioni mbili pia wameyakimbia makazi yao, idadi iliyovunja rekodi katika mizozo ya wakimbizi wa ndani barani Afrika.
Ghadhabu ndani ya nchi hiyo yaliyachochea majeshi kufanya mapinduzi na kumuondoa madarakani rais aliyechaguliwa Roch Marc Christian Kabore.
Soma pia:Burkina Faso yatangaza mpango mpana wa kupambana na mashambulizi ya itikadi kali