1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Burhan asema hawatashiriki mazungumzo ya amani

Hawa Bihoga
25 Agosti 2024

Mkuu wa Jeshi Sudan Abdel Fattah al-Burhan amesema serikali yake haitashiriki mazungumzo ya amani na kundi hasimu la wanamgambo nchini Uswisi, na badala yake ameapa "kupambana kwa miaka 100."

https://p.dw.com/p/4jtZz
Sudan | Mkuu wa Jeshi  Abdel Fattah al-Burhan
Mkuu wa Jeshi Sudan Abdel Fattah al-BurhanPicha: AFP

Al-Burhan ametoa msimamo huo wakati akizungumza na waandishi habari katika mji wa Port Sudan, kuhusu vita hivyo vilivyodumu kwa zaidi ya miezi 16 sasa.

Marekani ilianzisha mazungumzo nchini Uswisi mnamo Agosti 14 yenye lengo la kupunguza mateso kwa raia na kufikia usitishaji wa kudumu wa mapigano.

Soma pia:UN yasema iko tayari kupeleka chakula katika eneo la Darfur

Kujitokeza kwa ujumbe wa wanamgambo wa RSF kwenye mazungumzo hayo pamoja na muundo wake haukuridhisha jeshi la Sudan na kutangaza kutohudhuria mazungumzo hayo, ingawa lilikuwa likifanya mawasiliano ya simu na wapatanishi.

Mazungumzo hayo yalioandaliwa kwa pamoja na Saudi Arabia na Uswisi, huku Umoja wa Afrika, Misri, Umoja wa Falme za Kiarabu na Umoja wa Mataifa wakikamilisha kile kinachoitwa kundi la amani na kuokoa maisha nchini Sudan, ALPS.