1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ujerumani laidhinisha sheria za kudhibiti corona

18 Novemba 2021

Bunge la Ujerumani limeidhinisha sheria mpya kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona, wakati Kansela Angela Merkel anayekaimu serikali akijiandaa kukutana na viongozi wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/439fr
Deutschland | Sondersitzung des Bundestags zur Lage in Afghanistan
Picha: imago images/Achille Abboud

Bunge la Ujerumani limeidhinisha sheria mpya za kukabiliana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya Corona. Hatua hiyo imechukuliwa leo wakati Kansela Angela Merkel anayekaimu serikali, akijiandaa kukutana na viongozi wakuu wa majimbo 16 ya Ujerumani kujadili hatua zaidi za kukabiliana na janga la virusi hivyo. 

Janga la virusi vya Corona linatishia kuvuka viwango nchini Ujerumani-katika mkoa wa Bayern, Kusini mwa Ujerumani katika eneo la Freising, inaelezwa kwamba vitanda vya wagonjwa katika wodi za wagonjwa mahututi vimejaa na wafanyakazi wa huduma ya afya nao pia wamepungua.

Hospitali ya eneo hilo la Freising imefikia uamuzi ambao haukutarajiwa wa kumhamishia kaskazini mwa Itali mgonjwa mmoja wa Covid kwa ajili ya matibabu.Wakati maambukizi yakitajwa kuongezeka bunge la nchi hii limepiga kura na kupitisha sheria kadhaa leo Alhamisi zilizopendekezwa na vyama ambavyo vina uwezekano wa kuunda serikali ijayo ya shirikisho.

Soma Zaidi: Wimbi la 4 la corona laitikisa Ujerumani

Berlin | Debatte Bundestag zu Coronamaßnahmen | Angela Merkel
Kansela Angela Merkel anakutana na viongozi wakuu wa majimbo kujadili hatua zaidi za kupambana na janga hilo.Picha: Markus Schreiber/AP/picture alliance

Yapi yameidhinishwa?

Miongoni mwa yaliyopitishwa ni kutorefushwa kwa hali ya janga la kitaifa baada ya kipindi cha hali ya dharura ya kukabiliana na janga hilo kufikia mwisho wake hapo Novemba 25.

Kipindi hicho cha hali ya dharura cha kukabiliana na maambukizi ya virusi vya Corona nchini Ujerumani kilianzishwa mwezi March 2020 ambapo miongoni mwa mambo mengine kulikuweko na sheria kali za usafiri. Hata hivyo sheria zilizopitishwa na bunge sasa zitahitaji kuidhinishwa pia na Bundesrat ambalo ni  baraza la juu la maamuzi ya mwisho Ujerumani.

Aidha mpango wa kukabiliana na ongezeko la maambukizi unajumuisha sheria ya kuwalazimisha wafanyakazi wa vituo vya kuhudumia wazee pamoja na wageni wanaotembelea vituo hivyo kupima kila siku, haijalishi ikiwa mtu amechanja au hajachanja.

Tizama video:

Ujerumani yatahadharisha kuhusu ongezeko la maambukizi ya corona kwa wasiochanjwa

Kadhalika mtu atalazimika kuonesha uthibitisho wa ikiwa amechanjwa, amewahi kuugua Covid na kupona au kupima katika maeneo ya kazi na katika usafiri wa umma. Shule zitaendelea kuwa wazi na pia hakuna vizingiti vya kusafiri au watu kulazimishwa kuchanja. Lakini sheria kali imewekwa kwa wale watakaofanya udanganyifu wa vyeti vya chanjo ambapo adhabu ya hadi miaka mitano jela imewekwa. Kwa mujibu wa polisi ya Ujerumani suala la watu kughushi vyeti vya chanjo ni kubwa sana nchini Ujerumani ambapo kuna wanaouza vyeti hivyo vya bandia hadi yuro 400.

Nchini Uingereza shirika linalosimamia masuala ya usalama wa afya limesema watoto kati ya umri wa miaka 12 na 15 wanapaswa kucheleweshwa kuchanjwa endapo waliwahi kuugua Covid alau wiki 12 baada ya kuambukizwa. Uhispania nayo imetangaza kutoa chanjo ya ziada kwa wazee wa kuanzia umri wa miaka 60 na zaidi wakati Uholanzi ikisema inakabiliwa na upungufu wa vifaa vya upimaji virusi vya Corona.

Soma Zaidi:Maambukizi ya COVID-19 yaongezeka Ulaya na kuzusha hofu ya wimbi la nne 

Mashirika: DW

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW