Maambukizi ya COVID-19 yaongezeka Ulaya
4 Novemba 2021Hali hiyo inamesababisha kuwepo wito wa kulitaka Shirika la Afya Duniani, WHO kuchukua hatua za haraka baada ya kuelezea wasiwasi wake kuhusu uwezekano wa kuzuka wimbi la nne la maambukizi ya ugonjwa wa COVID-19.
Visa vya maambukizi vimeongezeka zaidi hasa Ulaya Mashariki na kusababisha mjadala iwapo zianzishe tena vizuizi vya kukabiliana na virusi vya corona kabla ya msimu wa sikukuu ya Krismasi na jinsi ya kuwashawishi watu kupata chanjo. Majadiliano hayo yanatokea wakati ambapo baadhi ya nchi za Asia, isipokuwa China zinafungua tena sekta ya utalii kwa ajili ya ulimwengu wote.
Kasi ya maambukizi yazusha hofu
Mkurugenzi wa WHO barani Ulaya, Dokta Hans Kluge amesema kasi ya maambukizi ya sasa katika nchi 53 za bara la Ulaya inaleta wasiwasi mkubwa. Kluge amesema virusi vya corona vinasambaa haraka katika miezi ya baridi wakati ambapo watu wanakusanyika nyumbani. Awali, afisa huyo wa WHO alionya kuwa iwapo Ulaya itafuata mkondo wake wa sasa, kunaweza kuwa na vifo 500,000 vinavyohusiana na COVID-19 ifikapo mwezi Februari.
''Kwa jumla, sasa kuna zaidi ya visa milioni 78 vilivyoripotiwa kwenye nchi za Ulaya, kuliko Asia Kusini na Mashariki, Mediterania Mashariki, eneo la Magharibi ya Bahari ya Pasifiki na Afrika kwa pamoja. Kwa mara nyingine tena tuko kwenye kilele cha maambukizi,'' alifafanua Kluge.
Bara la Ulaya limeshuhudia kuongezeka kwa visa vya maambukizi ya corona kwa asilimia 6 wiki iliyopita, huku kukiwa na takribani visa vipya milioni 1.8, ikilinganishwa na wiki moja kabla. Idadi ya vifo imeongezeka hadi asilimia 12 kwa kipindi hicho pia.
Ujerumani yenye uchumi mkubwa zaidi barani Ulaya imeripoti visa vipya 33,949 kwa siku, hilo likiwa ongezeko kubwa kushuhudiwa tangu kuzuka kwa janga la COVID-19 mwaka uliopita. Visa nchini Urusi na Ukraine pia vinazidi kuongezeka. Maambukizi mapya ya siku ya Austria yameonegezeka na kuizidi rekodi iliyowekwa mwaka mmoja uliopita.
Uingereza na kwengineko
Nchini Uingereza maambukizi ya virusi vya corona yameongezeka kwa kiwango cha juu zaidi kwa mwezi Oktoba, huku idadi ya visa vikiwa miongoni mwa watoto na eneo la kusini magharibi. Slovakia imeripoti visa vipya 6,713, huku maambukizi ya siku nchini Hungary yakiongezeka mara mbili zaidi na kufikia 6,268 ikilinganishwa na wiki iliyopita.
Poland yenye uchumi mkubwa zaidi Ulaya Mashariki leo imerekodi visa vipya 15,515, hiyo ikiwa idadi ya juu tangu mwezi Aprili. Croatia na Slovenia leo nazo pia zimerekodi maambukizi mapya ya kila siku. Romania ambako hospitali zimefurika wagonjwa wa COVID-19, Jamhuri ya Czech, Slovakia na Poland zimeimarisha sheria za kuvaa barakoa na kuanzisha hatua za kuzuia kuenea kwa virusi vya corona.
China pia iko katika tahadhari kubwa kwenye bandari za kuingia nchini humo katika juhudi za kupunguza hatari za maambukizi ya COVID-19 kutoka nje ya nchi na imeongeza vizuizi vya kuzuia maambukizi kusambaa, huku kukiwa na ongezeko la mripuko chini ya siku 100 kabla ya kuanza kwa michezo ya Olimpiki ya majira ya baridi itakayofanyika mjini Beijing.
(AFP, DPA, Reuters)