1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bunge la Ujerumani kujadili ulinzi wa Mahakama ya Katiba

10 Oktoba 2024

Wabunge wa Ujerumani watajadiliana kuhusu pendekezo la kuimarisha ulinzi wa Mahakama ya Katiba ya nchi hiyo Alhamis, wakati ambapo kuna wasiwasi kuhusiana na ongezeko la vyama kama Alternative für Deutschland AfD.

https://p.dw.com/p/4lcFI
Bunge la Ujerumani, Bundestag
Bunge la Ujerumani, BundestagPicha: Anna Ross/dpa/picture alliance

Pendekezo hilo lililowasilishwa na serikali ya muungano ya Kansela Olaf Scholz na chama cha upinzani cha Christian Democratic Union CDU, linalenga kuainisha ulinzi kwa mahakama hiyo katika katiba ya Ujerumani.

Hapo Jumatano, waziri wa haki Marco Buschmann aliashiria kuliunga mkono pendekezo hilo katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Ujerumani ARD.

"Tumeona nchini Poland na Hungary, mbinu zinazotumika kulemaza, kuharibu na kuzuia uhuru wa mahakama za katiba," alisema Buschmann.

Waziri wa Haki wa Ujerumani Marco Buschmann
Waziri wa Haki wa Ujerumani Marco BuschmannPicha: Britta Pedersen/dpa/picture alliance

Kwa sasa mahakama hiyo inaweza kufanyiwa mabadiliko endapo pendekezo la mabadiliko litapata uungwaji mkono wa wengi katika bunge la Ujerumani, Bundestag. Kwa upande mwengine katiba, inaweza kufanyiwa mageuzi tu endapo kutakuwa na uungwaji mkono wa thuluthi mbili katika mabunge yote.

Katika mpango huo mpya uliopüendekezwa, majaji watapewa muhula wa miaka 12 wa kuhudumu na watatakiwa kustaafu watakapofikia umri wa miaka 68, hilo likiwa litajumuishwa katika katiba.

Lakini Buschmann katika mahojiano menzine na shirika la habari la Ujerumani la Funke, ametahadharisha kwamba kupambana na wanasiasa wa siasa kali, si jukumu la kikatiba tu bali pia la kisiasa.