Bunge la seneti Marekani laishinda turufu ya Trump
2 Januari 2021Maseneta hao wameupitisha mswada wa sera ya ulinzi ambao Trump alikuwa ameupinga, wiki chache kabla kuondoka madarakani.
Walipokuwa wakikutana katika kikao cha nadra katika siku ya maadhimisho ya mwaka mpya, maseneta 81 dhidi ya 13 wamepiga kura na kupata thuluthi mbili inayohitajika ili kuishinda kura hiyo ya turufu.
Kura za turufu zilizopita za Trump ziliungwa mkono na seneti
Kulingana na sheria za Marekani, kura ya turufu ya rais ya kupinga mswadafulani inaweza kushindwa iwapo mswada unaojadiliwa unaungwa mkono na thuluthi tatu ya wabunge katika mabunge yote ya congress.
Kura nane za turufu za Trump zilizopita ziliungwa mkono na seneti.
Trump alikuwa amekataa kuutia saini na kuufanya kuwa sheria mswada huo wa matumizi ya ulinzi wa dola milioni 750 kwa kuwa ulikuwa haujaondoa sheria kadhaa za kulinda mitandao ya kijamii.
Wabunge wa Republican wapinga kuongezwa malipo kwa Wamarekani
Sababu yake nyengine ilikuwa kwamba mswada huo ulikuwa na kipengee kinachotoa nafasi ya kubadilishwa kwa majina ya kambi za jeshi, zilizokuwa zimepewa majina ya mejenerali walioongoza vikosi vya muungano wa majimbo ya kusini, yaliyokuwa yanaunga mkono utumwa, wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.
Wabunge wa Republican pia wamepinga shinikizo la wabunge wa Democratic kuongeza malipo ya misaada kwa Wamarekani kwa ajili ya virusi vya corona kutoka dola 600 hadi dola 2000. Rais Trump pia anaunga mkono nyongeza hiyo ya fedha.
Trump amekuwa haelewani na wabunge wa chama chake cha Republican tangu apoteze uchaguzi wa mwezi Novemba baada ya wengi wao kutomuunga mkono katika madai yake yaisokuwa na ushahidi ya wizi wa kura.