1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Trump atumia kura ya turufu kupinga azimio la bunge

Zainab Aziz Mhariri: Gakuba, Daniel
17 Aprili 2019

Rais Donad Trump ametumia kura ya turufu kupinga azimio la bunge la nchi yake linaloitaka Marekani iache kuisaidia Saudi Arabia katika vita vya Yemen.

https://p.dw.com/p/3GxWe
USA, Washington: Trump legt Veto gegen Resolution zu US-Militärhilfe im Jemen ein
Picha: Getty Images/Z. Gibson

Spika Pelosi amesema kura ya turufu ya Rais Trump itaendeleza aibu ya Marekani ya kuhusika na mgogoro  wa nchini Yemen. Trump alitumia kura hiyo hapo jana kuzuia azimio la bunge lenye lengo la kukomesha msaada wa kijeshi wa Marekani kwa Saudi Arabia. Azimio hilo liliungwa mkono na baraza la Wawakilishi  pamoja na baraza la Seneti.

Hii ni mara ya pili kwa Trump kutumia Kura ya turufu kupinga azimio la  bunge.  Na ili kuibatilisha kura ya Rais, thuluthi mbili ya wabunge watahitajika jambo ambalo kwa sasa haliwezekani katika bunge lililogawika kwa kiwango kikubwa.

Kwa kuipinga sera ya mambo ya nje ya Rais Donald Trump, Chama cha  Democtratic mnamo siku ya Jumatatu kilipitisha azimio la kuutaka utawala wa Trump kusitisha kuiunga mkono Saudi Arabia katika vita vya nchini Yemen.

Spika wa Bunge. Nancy Pelosi aliwaambia waandishi wa habari kwamba kutiwa saini muswada huo ni kutekeleza wajibu wa bunge katika kusimamia matumizi ya kijeshi .

Kupitishwa kwa azimio hilo na pande  zote mbili za bunge kulizingatiwa kuwa hatua ya kihistoria kwa  sababu hii ni mara ya kwanza kwa mswada wa bunge wa kupinga vita kuwasilishwa kwa Rais kwa mujibu wa sheria inayohusu vita iliyopitishwa mnamo  mwaka 1973.

Spika wa Bunge la Marekani Nancy Pelosi
Spika wa Bunge la Marekani Nancy PelosiPicha: picture-aliance/AP Photo/J. S. Applewhite

Hata hivyo uamuzi wa Rais Trump siyo wa kushangaza. Rais Trump ameiunga mkono thabiti Saudi Arabia  hata baada ya mwandishi habari Jamal Khashoggi kuuliwa na hata baada ya idara za ujasusi  za Marekani  kubainisha kwamba mrithi wa mfalme wa Saudi Arabia Mohammed alihusika na mauaji.

Umoja wa Falme za Kiarabu umesifu na kuuita mkakati  wa Rais Donald Trump wa kutumia kura ya turufu kulipinga azimio la bunge lililomtaka asimamishe msaada wa Marekani kwa ajili ya vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia huko nchini Yemen.

Waziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu Anwar Gargash ambaye serikali yake ni mshirika muhimu wa Saudi Arabia katika vita vya Yemen ameandika kwenye mtandao wa Twitter kwamba hiyo ni ishara nzuri ya Marekani ya kuwaunga mkono washirika wake. 

Akitetea uamuzi wake Rais Trump amesema azimio hilo la wabunge halikuwa la lazima. Amesema azimio  hilo ni juhudi za hatari za kudhoofisha mamlaka yake ya kikatiba, hatua ambayo ameeleza inahatarisha  maisha ya raia wa Marekani pamoja na ya wanajeshi jasiri wa nchi hiyo. Rais Trump pia amehoji kwamba azimio la bunge lingeathiri sera ya nje ya  Marekani na kuathiri uhusiano wa Marekani na Saudi Arabia.

Trump ameeleza kwamba mazungumzo yatahitajika ili kuleta Amani nchini Yemen na amesisitiza kuwa  Marekani haihusiki na mapigano moja kwa moja nchini Yemen,ila tu dhidi ya magaidi wa kundi la  Al-Qaeda.

Vyanzo: /AFP/AP/p.dw.com/p/3GvtN