1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Buhari akutana na viongozi jirani

Admin.WagnerD11 Juni 2015

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, leo amekutana na viongozi wenzake wa nchi jirani kujadili mikakati ya kijeshi ya kulitokomeza kundi la uasi la Boko Haram.

https://p.dw.com/p/1Ffqo
Niger Buhari Issoufou
Picha: DW/M. Kanta

Rais wa Nigeria Muhammadu Buhari, amekutana leo na viongozi wenzake wa kikanda mjini Abuja katika mazungumzo ya kuunda kikosi cha pamoja dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram. Hii ikiwa ni mojawapo ya jitihada zake za awali kama rais mpya wa nchi hiyo.

Rais huyo mwenye umri wa miaka 72, na ambaye aliapishwa rasmi wiki mbili zilizopita aliwakaribisha viongozi wenzake kutoka nchi za Chad, Niger na Benin katika mkutano wa ghafla wa siku moja uliofanyika ndani ya uwanja wa ndege wa Abuja. Cameroon hata hivyo imetuma waziri wake wa ulinzi.

Kuhusu pendekezo lililotolewa. la kupokezana uongozi wa mapambano hayo baina ya nchi hizo tano. Buhari amesema hilo linaweza kuidhoofisha operesheni hio, na kupendekeza badala yake itakuwa vizuri kwa Nigeria kuongoza kikosi hicho cha kupambana na wanamgambo wa Boko Haram kwa muda wote wa operesheni hiyo.

Symbolbild Soldaten Nigeria
Wanamgambo wa kundi la Boko HaramPicha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Buhari amewaambia waandishi habari kuwa Nigeria imeahidi kiasi cha dola milioni 100 kuanzisha kikosi hicho, ambacho kitakuwa na kambi yake katika mji mkuu wa Chad Ndjamena lakini kitaongozwa na Nigeria.

Uvamizi wa kundi la Boko Haram

Kundi la Boko Haram hadi sasa limeshauwa maelfu ya watu na kusababasha watu milioni 1.5 kupoteza maakazi yao, katika kipindi cha miaka sita ya uasi. Wenye lengo la kuanzisha dola la kiislamu, katika maeneo ya kaskani mashariki mwa Nigeria.

Kabla ya Chad, Niger, Cameroon na Nigeria kuzindua mapambano dhidi ya Boko Harama mwaka huu, kundi hilo lenye mafungamano na kundi kigaidi la Dola la Kiislamu IS lilikuwa linadhibiti maeneo yenye ukubwa wa nchi nzima ya Ubelgiji.

Kupambana na uasi ni moja wapo ya ahadi za kampeni ya Buhari ikilinganishwa na mtangulizi wake Goodluck Jonathan, aliyelaumiwa kwa uzembe hasa baada ya kutekwa nyara kwa wasichana 200 katika shule ya Chibok aprili ya mwaka jana.

Wakati mkutano huo ulipokuwa ukiendelea, polisi wa Nigeria wameripoti wanawake watatu waliokuwa wamevaa mikanda ya miripuko wamejiripua katika shambulizi wa kujitoa muhanga mjini Maiduguri kaskazini mashariki mwa NIgeria. Watu kadhaa wameuwawa katika mashambulizi ya kujitoa muhanga, katika wiki zilizopita yanayosemekana yalifanywa na kundi la Boko Haram.

Afisa mmoja wa polisi aliyakataa kutajwa jina amesema katika uchunguzi wao wamegundua kuwa wengi wa wasichana, wanaojitoa muhanga kwa kujiripua kwa mabomu wanakuwa hawana udhibiti nayo kwani yanaripuliwa kutoka mbali kwa kutumia kifaa maalumu.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/RTRE/AFP/AP

Mhariri:Josephat Charo