Bomu lauwa wawili, lajeruhi saba kambi ya wakimbizi Goma
5 Aprili 2024Picha zilizosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuanzia usiku wa Jumatano (Aprili 4) ziliwaonesha watu wawili waliouawa na wengine waliojeruhiwa wakiwa wamelazwa chini na wakitokwa na damu.
Katika mahojiano na DW, afisa mkuu wa kambi hiyo ya ya Shabindu iliyo viungani mwa mji wa Goma, Mhima Binwa, alieleza kuwa hali iliendelea kuwa ya wasiwasi katika kambi hiyo ya watu waliokimbia mapigano kati ya jeshi la serikali na waasi wa M23.
"Ilikuwa ni majira ya saa 2:30 usiku wakati mtu mwenye silaha aliporipua guruneti na kusababisha vifo vya watu wawili na wengine saba kujeruhiwa vibaya na ambao wamepelekwa hospitalini kwa ajili ya kupata matibabu." Alisema Binwa.
Soma zaidi: Jeshi la Kongo lazima jaribio la M23 kuutwaa mji wa Sake
Mji wa Goma pamoja na viunga vyake umeshuhudia ongezeko kubwa la vifo vya raia katika kambi za wakimbizi zinazolengwa na mabomu tangu januari mwaka huu baada ya waasi wa M23 kuzidisha mashambulizi.
Baadhi ya kambi za wakimbizi wa ndani katika mji wa Goma zimegeuka kuwa mahala hatari kutokana na watu wanaorandaranda ovyo wakiwa na silaha na ambao, kulingana na vyanzo vya kiraia, ni vijana wanaojiita "Wazalendo."
Mabomu na mashambulizi ovyo ovyo
Vijana hao wanaripotiwa kufyatua risasi kila jioni ndani na nje ya kambi za wakimbizi, kwa mujibu wa Akonkwa Safari, mwanaharakati wa haki za binaadamu mkoani Kivu Kaskazini.
"Tunahuzunishwa sana na hali mbaya ya usalama kufuatia mauwaji ya watu wasiokuwa na hatia, wakiwemo wakimbizi. Enyi viongozi wa serikali ndio muda huu wa kubeba dhamana kwa sababu watu wamechoshwa sasa na hali hii", alisema mwanaharakati huyo. .
Baadhi ya wakaazi wa Goma wanaoathirika na hali hiyo ya ukosefu wa usalama waliiambia DW kwamba kila ikiingia jioni, wanapatwa na wasiwasi wa maisha yao.
Soma zaidi: Kikosi cha EAC chaanza kuondoka kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo
"Kama wakaazi wa Goma tunaogopa sana kila ikitimu jioni, kwa sababu watu wenye silaha wanazungukazunguka kila mahali wakirusha risasi kiholelea bila kujali usalama wetu", alisema mmoaj wao.
Mbali na viunga vya mji wa Goma, mabomu mengine yalianguka kwenye vijiji vya Mubambiro na Nzulo wilayani Masisi vilivyo karibu kilometa 20 kutoka mji wa Goma na ambako hali ya usalama imeendelea kuwa mbaya zaidi.
Kulingana na taarifa iliyotolewa na idara ya serikali inayoshughulikia mabomu yaliyotegwa ardhini (SYLAM), takribani watu 33 wameuawa na wengine 74 wamejeruhiwa na mabomu hayo yaliyotupwa na waasi wa M23 katika maeneo yanayokaliwa na wakaazi katika kipindi cha miezi minne kuanzia Januari mwaka huu.