Vyombo hivyo vya usalama vimedai kuwa na taarifa kuwa akiwa huru, Bobi Wine anapanga kuwachochea vijana kishiriki katika ghasia.
Tangu kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi, Bobi Wine na viongozi wa chama chake cha NUP wamepinga hatua ya tume ya uchaguzi kumtangaza rais Yoweri Museveni kuwa mshindi.
Kulingana na wasemaji wa majeshi na polisi wamepata taarifa za kuaminika kuwa makundi ya vijana walikuwa wameandaliwa kufanya vurugu kwenye barabara kuu za kuingia na kutoka mji wa Kampala na ndiyo sababu kubwa ya kuhakikisha kuwa uvunjaji sheria wa aina hiyo hautokei.
Chama hicho kinahoji kwa nini matokeo kutoka vituo 1,257 hayakujumuishwi kwenye matokeo hayo huku vituo 271 kati ya hivyo vikiwa katika wilaya ya Wakiso ambayo ni ngome kuu ya Bobi Wine.
Chama cha NUP kinalenga kuupinga ushindi wa Museveni
Chama hicho sasa kinaandaa ushahidi kuwasilisha rufaa mahakamani kupinga matokeo hayo. Lakini kisa cha majeshi na polisi kuvamia makao makuu ya chama hicho asubuhi ya Jumatatu na kuwazuia watu kuingia wala kutoka kimetajwa kuwa kitakwaza shughuli ya kukusanya ushahidi wanahitaji kuwasilisha mahakamani.
Wakati huohuo, polisi imethibitisha kuwa watu wanne akiwemo mama mjamzito wamepoteza maisha yao kufuatia ghasia zilizozuka mjini Masaka kusini mwa nchi baada matokeo ya urais kutangazwa.
Wagombea wengine wa urais nao wamepinga matokeo hayo hasa kwa kudai kuwa idadi ya wapiga kura ilikuwa kubwa kuliko ile ya watu milioni 10 hivi waliotajwa kushiriki.
Kulingana na tume ya uchaguzi waliosajiliwa kupiga kura ni watu zaidi ya milioni 18.