Museveni ashinda muhula wa sita madarakani
16 Januari 2021Kulingana na mkuu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Uganda, Simon Mugenyi Byabakama, asilimia 57,22 ya Waganda takribani milioni 18 waliojisajili kupiga kura waliitikia zoezi hilo la Januari 14.
Soma zaidi: Bobi Wine: Jeshi limezingira makazi yangu, niko mashakani
Amesema Museveni amepata asilimia 58.6 ya kura zote, akifuatiwa na Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine aliyepata asilimia 34.8. Kati ya wagombea wengine 9 wa urais hakuna aliyefikisha hata asilimia tano.
Byabakama amewataka raia wa Uganda kubaki watulivu na kuyakubali matokeo ya uchaguzi, na kuhimiza wale wanaosherehekea ushindi kuheshimi masharti ya kujikinga na ugonjwa wa COVID-19.
Miaka 40 kileleni mwa siasa za Uganda
Museveni aliyeingia madarakani mwaka 1986 baada ya kundi la waasi aliloliongoza kuyashinda majeshi ya serikali, akimaliza muhula huu atakuwa ameiongoza Uganda kwa miaka 40, na kuwa miongoni mwa marais waliodumu mamlakani kwa muda mrefu zaidi barani Afrika.
Wakati Tume ya Taifa ya Uchaguzi ikiyatangaza matokeo hayo mchana Jumamosi, makaazi ya Bobi Wine yaliyoko nje kidogo ya mji mkuu, Kampala yalikuwa yamezingirwa na wanajeshi. Ingawa chama chake kinasema hali hiyo ni kama kumweka katika kifungo cha nyumbani, serikali inadai ni katika juhudi za kuhakikisha usalama wake.
Soma zaidi: Maoni: Uchaguzi wa Uganda ni fursa iliyopotea
Uchaguzi huu ulifanyika baada ya kutokea ghasia mbaya zaidi kuundama uchaguzi wa Uganda, ambapo watu 54 waliuawa, viongozi kadhaa wa upinzani kukamatwa na vyombo vya habari kufungiwa matangazo.
Wakati serikali ikisema uchaguzi ulifanyika katika mazingira salama, Boni Wine amesema ulijaa visa vya wizi wa kura na vurugu, akidai katika baadhi ya vituo mawakala wake walipigwa na kufukuzwa wasiweze kufuatilia kilichokuwa kikiendelea.
Bobi Wine ayapinga matokeo
Hapo jana alisema ''chochote kinachotangazwa ni upuuzi mtupu, na tunakikataa na kujitenga nacho.''
Msemaji wa chama chake cha National Unity Platform (NUP) Joel Ssenyonyi, amsema hawawezi kuondoa uwezekano wa wafuasi wao kupinga matokeo yaliyotangazwa.
''Watu wana hasira kwa sababu kura zao zimeibiwa,'' amesema Ssenyonyi, na kuongeza kuwa yeye na Bobi Wine hawana haja ya kuwaelekeza namna ya kukasirika. ''Hata hatuwezi kuwadhibiti'', ameongeza.
Soma zaidi: Museveni aongoza matokeo ya awali nchini Uganda
Mwanadiplomasia mwandamizi wa Marekani barani Afrika Tobor Nagy amewataka wadau wote katika uchaguzi wa Uganda kujizuia kufanya vurugu, na kutaka mawasiliano ya intaneti na mitandao ya kijamii kufunguliwa. Mawasiliano hayo yamezimwa nchini Uganda kwa muda wa siku nne zilizopita.
Msemaji wa serikali mjini Kampala, Ofwono Opondo amesema intaneti ilizuiliwa ili kuepusha matumizi yake mabaya, yakiwemo kueneza taarifa za uongo kwa lengo la kuhujumu uhalali wa mchakato wa uchaguzi.
Vyanzo: afpe, dpae