Bobi Wine aondosha kesi ya kupinga ushindi wa Museveni
22 Februari 2021Robert Kyagulanyi almaarufu Bobi Wine aliwasilisha kesi katika mahakama ya juu tarehe mosi mwezi huu akipinga hatua ya rais Museveni kutangazwa kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais uliopita, kwa kupata asli mia 58 ya kura dhidi yake ambaye alitangazwa kupata asli mia 35 hivi.
Katika kipindi cha wiki mbili amewasilisha shauri katika mahakama hiyo akitaka kuongeza ushahidi zaidi ambao anaelezea ungeweka bayana malalamiko yake kwamba palitokea udanganyifu mkubwa katika uchaguzi sambamba na kutokuwepo na usawa katika mchakato wote wa uchaguzi. Ila mahakama hiyo ilitupilia mbali maombi yake.
soma zaidi:Bobi Wine awasilisha mahakamani rufaa iliyorekebishwa
Ni kwa msingi huu ndipo ameelezea kuwa hana imani na mahakama hiyo kutoa maamuzi ya haki pamoja na kumtaja jaji mkuu kudhihirisha kuwa hawezi kufikia maamuzi kwamba rais Museveni si mshindi halali.
Bobbi Wine kuweka hadharani ushahidi uliokataliwa na mahakama ya juu
Bobi Wine ameongezea kuwa atauweka wazi kwa umma ushahidi uliokataliwa ili wafahamu kwa nini mahakama hiyo pamoja na upande wa rais Museveni walipinga kuwasilishwa kwake katika kufikia maamuzi ya kesi hiyo.
soma zaidi:Museveni ashinda muhula wa sita madarakani
Mara tu baada ya kupokea habari za Bobi Wine kuondoa kesi hiyo, wakili Oscar Kihika ambaye anaongoza timu ya mawakili wa chama cha NRM pamoja na rais Museveni ameonya kuwa mwanasiasa huyo atajutia gharama atakazotakiwa kuwafidia kwa hatua hiyo.
Hata hivyo, Bobi Wine amesisitiza kuwa hatababaishwa na mawakili hao na yuko tayari kwa chochote kitakachotokea.
Mwandishi: Lubega Emmanue DW Kampala