Blinken azuru Saudi Arabia kujenga mahusiano yaliyoharibika
6 Juni 2023Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken ameelekea Saudi Arabia kuimarisha mahusiano yaliyodhoofika na mshirika wake huyo wa muda mrefu. Ziara hiyo inajiri wakati taifa hilo la kifalme lenye utajiri wa mafuta likiimarisha mahusiano na wapinzani wa Marekani. Ziara ya Blinken ya siku tatu pia itaangazia juhudi za kuumaliza mizozo ya nchini Sudan na Yemen, vita vya pamoja dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu na mahusiano ya ulimwengu wa Kiarabu na Israel.Ziara ya Blinken Saudi Arabia, ina lengo gani?
Ziara yake inajiri katika wakati ambao kuna mabadiliko ya miungano katika Mashariki ya Kati, yanayojikita katika maelewano yaliyofikiwa kati ya madola makubwa ya kikanda Saudi Arabia na Iran kwa usimamizi wa China. Blinken anatarajiwa kutua katika mji wa Bahari ya Shamu wa Jeddah jioni hii na kukutana na kiongozi wa Saudia Mwanafalme Mohammed bin Salman, kabla ya kuelekea Riyadh hapo kesho kwa mkutano wa Baraza la Ushirikiano wa Nchi za Kiarabu.