Ziara ya Blinken Saudi Arabia, ina lengo gani?
6 Juni 2023Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken anatarajiwa kukutana na maafisa wa ngazi za juu wa utawala wa kifalme wa Saudi Arabia na vile vile huenda akakutana pia na mrithi wa kiti cha ufalme, Mohammed Bin Salman mjini Riyadh.
Dhamira hasa ya ziara ya Blinken ni kuimarisha mahusiano na utawala wa Riyadh baada ya kuonekana kuongezeka mivutano kwa miaka kadhaa baina ya pande hizo kuhusu masuala mbali mbali tangu,Iran mpaka usalama wa kikanda hadi suala la bei ya mafuta.
Hii ni ziara ya pili ya mjumbe wa ngazi za juu kutoka serikali ya Marekani kuitembelea Saudi Arabia baada ya ile iliyofanywa Mei 7 na Jake Sullivan,mshauri wa masuala ya usalama wa taifa wa ikulu ya Marekani.
Ziara ya Blinken itakwenda mpaka tarehe 8 na imekuja siku kadhaa baada ya serikali ya Riyadh kutangaza kwamba inadhamiria hasa kupunguza tena uzalishaji mafuta kuanzia mwezi Julai,hatua ambayo inawezekana ikaongeza zaidi mvutano katika mahusiano baina ya nchi hizi mbili,ambao toka hapo ni wa mashaka kufuatia kunyooshewa kidole rikodi ya haki za binadamu ya Saudi Arabia pamoja na mikwaruzano kuhusu sera ya Marekani kuelekea Iran.
Miongoni mwa malengo ya ziara hii ni pamoja na kurudisha tena ushawishi kwa utawala wa riyadh kuhusiana na suala la bei za mafuta,kupunguza ushawishi wa China na Urusi kwenye kanda hiyo pamoja na kutafuta matumaini ya hatimae kurudi kwa mahusiano ya kawaida kati ya Saudi Arabia na Israel
Imeelezwa kwamba kwa sehemu ziara hii ni ya kutafuta majadiliano ya uwezekano wa Saudi Arabia kujiunga kwenye kile kinachoitwa ''Mapatano ya Abraham''yaliyokamilishwa kipindi cha utawala wa Donald Trump kati ya Israel,Umoja wa falme za kiarabu,Bahrain na Morocco.
Kwa upande mwingine raia wa Marekani na wakaazi wenye jamaa zao wanaozuiliwa jela nchini Saudi Arabia wamemtaka waziri huyo wa mambo ya nje kupitia barua kuwashinikiza maafisa wa nchi hiyo kuwaachia huru mara moja.
Miongoni mwa wanaoshikiliwa na utawala wa riyadh ni pamoja na ulamaa maarufu Salman al-Odah,watoto wa aliyekuwa mkuu wa ujasusi Saad al Jabri,na mtetezi ya haki za binadamu Mohammed al Qahtani na mfanyakazi wa shughuli za kutoa msaada Abdulrahman al Sadhan.
Soma pia: Biden kusitisha mauzo ya silaha UAE na Saudi Arabia
Saudi Arabia iliwahi kuwaachia huru raia kadhaa wa Marekani lakini ikawapiga marufuku baadhi yao kutosafiri nje ya Saudi Arabia.
Ama pia ziara ya Blinken imekuja siku moja baada ya rais wa Venezuela Nicolas Maduro kukaribishwa Riyadh jana Jumatatu ambako alikutana na Mwanamfalme Mohamed Bin Salman huko Jeddah na kuwa na mazungumzo leo Jummanne katika kasri la Al Salam.
Mazungumzo yao yalijikita kutathmini mahusiano ya nchi zao,uwezekano wa kushirikiana na pamoja na kujadili fursa zilizopo kwa pande zote.