Blinken azuru mataifa ya Afrika Magharibi
23 Januari 2024Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Marekani ataanza ziara yake nchini Cape Verde kabla ya kuzuru Ivory Coast, Nigeria na Angola, hii ikiwa ziara yake ya kwanza kusini mwa jangwa la Sahara katika kipindi cha miezi 10, huku akiachana kwa muda na ufuatiliaji wake katika mgogoro kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza.
Marekani kuonesha upande wa kirafiki kwa Afrika
Huku Waafrika wengi wakitilia shaka umakini wa Marekani kwa Mashariki ya Kati na Ukraine,na kwa Rais Joe Biden kushindwa kutimiza ahadi ya kulitembelea bara la Afrika mwaka wa 2023, Blinken atajaribu kuonesha upande wa kirafiki wa Marekani wakati wa ziara hiyo.
Masuala yatakayoangaziwa na Blinken
Molly Phee, mwanadiplomasia mkuu wa Marekani katika bara la Afrika, amesema kuwa Blinken anatazamia kuzisaidia nchi katika eneo hilo la Sahelkuimarisha jamii zao na kuzuia kuenea kwa vitisho vya kigaidi vinavyoshuhudiwa .
Phee amewaambia waandishi wa habari kwamba Blinken atazihimiza nchi kuweka kipaumbele kwa usalama wa raia zinapofanya operesheni za kijeshi, na kuimarisha haki za binadamu na maendeleo ya jamii, hasa miongoni mwa jamii zilizotengwa.
Soma pia: Blinken anatarajiwa kufanya ziara barani Afrika na kutembelea mataifa manne
Mwanadiplomasia huyo ameongeza kuwa Blinken atapongeza udumishaji wa demokrasia nchini Ivory Coast chini ya Rais Alassane Ouattara, mchumi aliyesomea Marekani ambaye ameazimia kushughulikia migogoro ya wenyewe kwa wenyewe iliyodumu kwa mwongo mmoja tangu alipochaguliwa kwa mara ya kwanza mwaka 2010.
Ivory Coast haijashuhudia mashambulizi makubwa ya kigaidi kwa takriban miaka miwili.
Blinken kuhudhuria mechi ya michuano ya AFCON
Baadaye leo jioni, Blinken anatarajiwa kuhudhuria mechi ya michuano inayoendelea ya Kombe la Mataifa ya Afrika AFCON mjini Abidjan, siku chache baada ya ziara ya waziri wa mambo ya nje wa China nchini Ivory Coast, ambayo Washington inaiona kuwa mpinzani wake mkuu wa muda mrefu na ambayo imeongeza ushawishi wake barani Afrika katika miongo miwili iliyopita.
Utafiti wafichua mbinu zinazotumiwa na uongozi wa Ouattara
Utafiti wa mwaka jana uliofanywa na Kundi la Kimataifa linalofuatilia Migogoro ulitaja mbinu mbili zinazotumiwa chini ya Ouattara ya kupeleka vikosi karibu na mipaka ya Mali na Burkina Faso lakini pia kuwekeza katika maendeleo ya kiuchumi ya Kaskazini mwa Ivory Coast, kwa kuzingatia kutoa fursa kwa vijana na kuwawezesha wanawake.
Phee amesema Marekani inafahamu kuwa Ivory Coast bado ina hofu kuhusu usalama kutokana na eneo lake kijiografia.
Soma pia:Blinken azungumza na Bazoum kwa njia ya simu
Mwaka jana, utawala wa Biden ulitangaza mpango wa miaka 10 kuhimiza udhibiti na kuzuia mapigano katika mataifa ya Benin, Ghana, Guinea, Ivory Coast na Togo.
Wakati wa ziara yake yake ya mwisho katika eneo hilo mnamo Machi 2023, Blinken alikuwa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu zaidi wa Marekani kuwahi kufanya ziara nchiniNigerakitumai kuonesha uungaji mkono kwa rais mteule Mohamed Bazoum.
Miezi minne baadaye, jeshi la nchi hiyo lilipindua uongozi wa Bazoum, na wiki iliyopita, waziri mkuu aliyeteuliwa na mamlaka hiyo ya kijeshi alifanya ziara nchini Urusi kutafuta ushirikiano mkubwa zaidi.