1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaNiger

Blinken aelekea Niger kuonyesha mshikamano zaidi wa Marekani

Sylvia Mwehozi
16 Machi 2023

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken anaelekea nchini Niger katika ziara ya nadra, akiwa ametokea nchini Ethiopia ambako alisifu maendeleo katika utekelezaji wa mkataba wa amani wa kumaliza mzozo wa Tigray.

https://p.dw.com/p/4OkzE
Äthiopien USA Demeke Hasen Antony Blinken
Picha: Ethiopian Foreign Ministry

Blinken anakuwa mwanadiplomasia wa kwanza wa ngazi ya juu kuwahi kuitembelea Niger ambayo ni koloni la zamani la Ufaransa na kambi muhimu ya kijeshi kwa vikosi vya Magharibi vinavyopambana na wapiganaji wa jihadi katika kanda iliyokumbwa na machafuko ya Sahel. Blinken anatarajiwa kutangaza msaada zaidi wa Marekani kwa Niger, moja ya nchi maskini duniani.

Akizungumza nchini Ethiopia siku ya Jumatano, Blinken alisema ziara yake katika nchi hizo mbilini sehemu ya ahadi ya Rais Joe Biden ya kushikamana kikamilifu na Afrika. Blinken amesifu maendeleo katika utekelezaji wa mkataba wa amani wa kukomesha mzozo wa Tigray, lakini hakugusia juu ya kuirejesha Ethiopia katika mpango wa biashara na Marekani.

Äthiopien | Permierminister Abiy Ahmed und Anthony Blinken
Blinken na Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy AhmedPicha: Fana Broadcasting Corporate S.C

Baada ya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed na kiongozi mkuu wa chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray TPLF Getachew Reda, Blinken alisema makubaliano hayo ya amani yamesaidia "kupungua kwa kiasi kikubwa" kwa unyanyasaji. Aidha, mwanadiplomasia huyo aliitaka Ethiopia kuhakikisha inawajibika kwa ukiukaji wa haki katika vita vya kikatili vya Tigray, akisema ni muhimu katika kuanzisha tena ushirikiano mkubwa wa kiuchumi na mshirika wake wa muda mrefu.

"Kupata haki na kuwaleta watu pamoja, hiyo ndiyo njia ya kuhakikisha kuwa amani inadumu na watu wanaendelee na maisha yao na nchi inaweza kusonga mbele," alisema Blinken. 

Kabla ya kuelekea Niger Blinken amefanya mazungumzo na uongozi wa Umoja wa Afrika kama sehemu ya juhudi za utawala wa Biden wa kuonyesha heshima kwa Afrika na kuepuka dhana ya jukumu kubwa la Marekani.

Äthiopien Addis Abeba | US-Außenminister Antony Blinken besucht UN-Logistikzentrum
Blinken alitembelea ghala la Umoja wa Mataifa mjini Addis AbabaPicha: Tiksa Negeri/REUTERS

Mazungumzo yaliyoongozwa na Umoja wa Afrika na kuungwa mkono na wanadiplomasia wa Marekani yaliwezesha makubaliano ya usitishaji mapigano mnamo mwezi Novemba ambayo kwa kiasi kikubwa yamekomesha vita vya kikatili vya miaka miwili huko Tigray kaskazini mwa Ethiopia.

Utawala wa Biden ulizindua kampeni kubwa ya ushiriki wake Afrika katikati mwa kutanuka kwa uwekezaji wa China, inayoonekana kama mshindani mkuu kwa Marekani, lakini sasa pia kuna wasiwasi wa Urusi.Marekani na Ethiopia wajadili uwajibikaji huko Tigray

nchi ya Mali ambayo ni jirani ya Niger imeingia katika mzunguko wa Urusi kwa kuajiri  kundi la mamluki la Wagner, baada ya vikosi vya Ufaransa kuondoka kufuatia miaka tisa ya operesheni ya kijeshi ambayo ilizuia udhibiti wa wapiganaji wa jihadi, lakini ilipoteza ushawishi baada ya mapinduzi ya mfululizo.

Mwezi uliopita Mali ilikuwa nchi mojawapo kati ya sita zilizoungana na Urusi kupiga kura dhidi ya azimio la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lililoitaka Moscow kujiondoa Ukraine katika maadhimisho ya mwaka mmoja ya uvamizi huo.