Bingwa wa marathon Kelvin Kiptum afariki kwa ajali Kenya
12 Februari 2024Wananchi wa Kenya wanaomboleza kifo cha mwanariadha Kelvin Kiptum ambaye maisha yake yamekatizwa na ajali ya barabarani katika barabara kuu ya Eldoret-Ravine. Ajali hiyo ilitokea baada ya gari lake kupoteza mwelekeo na kugonga mti mkubwa kando ya barabara.
Kwa mujibu wa Kamanda wa polisi wa kaunti ya Elgeyo Marakwet, Kenneth Kimani bingwa huyo wa mashindano Chicago Marathon alipata ajali alipokuwa akirudi nyumbani kwake mjini Eldoret mwendo wa saa tano usiku wa Jumapili.
"Jumapili usiku ajali ilitokea katika barabara Eldoret-Ravine Mwisho wa siku ya Jumapili, gari yenye usajili wa nambari KDL 566F, Toyota Premio, kulikuwa na abiria watatu mmoja wao Kelvin Kiptum, bingwa wa Chicago Marathan,” alisema Kamanda wa Polisi wa Keiyo Kusini Abdullahi Dahir katika taarifa kuhusiana na ajali hiyo.
Soma pia: Kiptum atahadharishwa baada ya kuvunja rekodi ya dunia
Dahir aliongeza kuwa mwanamke aliyekuwa nyuma ya gari hilo kwa jina Sharon Kosgei alipata majeraha na kutibiwa kwenye hospitali moja mjini Eldoret. Sharon ameruhusiwa kuondoka hospitalini.
"Nilikuwa narudi nyumbani, nilipofika makutano nikasikia mtu anapiga kelele, kufika hapo nikaona gari, nikatafuta namba za OSC nikampigia simu, akaniambia hatua itachukuliwa,” alisema Fredrick Mutai, muhudumu wa magari ya uchukuzi wa umma ambaye alikuwa mmoja wa watu wa kwanza kufika kwenye eneo la mkasa.
Mwisho wa safari
Kiptum, mzaliwa wa eneo la mwinuko wa Kenya ambalo limetoa wakimbiaji wengi mashuhuri duniani wa mbio za masafa marefu, alianza kushiriki mbio za kimataifa kwenye mzunguko wa nusu-marathon mwaka wa 2019.
Aliingia kwa kasi katika mbio kamili za urefu wa kilomita 42.195 kwa kuweka rekodi ya nne ya kasi kubwa zaidi ya 2.01.53 na kushinda Marathon ya Valencia ya 2022 akiwa anashiriki kwa mara ya kwanza.
Mbio hizo ziliweka wazi mkakati wake wa mbio ndefu, ambapo alikuwa anakimbia na kundi kwa kilomita 30 za kwanza na kisha kuongeza kasi na kukimbia peke yake kwa muda uliosalia wa mbio.
Soma pia:Kiptum aivunja rekodi ya London Marathon
Alitumia mbinu zilezile kushinda London Marathon Aprili iliyopita katika rekodi ya mwendo wa saa 2:01:25 na tena mjini Chicago mwezi Oktoba kwa kupunguza sekunde 34 kwenye rekodi ya dunia ya Kipchoge.
Hizo ndiyo zilikuwa mbio zake za mwisho kabla ya kifo chake cha ghafla, ambacho kilikuja wiki moja tu baada ya shirika la Riadha Duniani kuidhinisha rekodi yake ya dunia.
Hakizimana, 36, alikuwa mwanariadha wa zamani wa masafa marefu ambaye bado anashikilia rekodi ya Rwanda ya mbio za mita 3,000 za kuruka viunzi. Alikutana na Kiptum mara ya kwanza alipokuwa akifanya mazoezi katika Bonde la Ufa na alifanya kazi naye kwa bidii kabla ya mbio za marathon za London mwaka jana.
"Nimeshtushwa na kuhuzunishwa sana kujua kifo cha Kelvin Kiptum na kocha wake Gervais Hakizimana," bingwa wa Olimpiki wa Kenya mara mbili na mshikilizi wa rekodi ya dunia ya mita 800 David Rudisha alisema kwenye X.
"Hii ni hasara kubwa."