Bila wapinzani mkutano wa Geneva hauwezekani
2 Novemba 2013Akitaraji kuendeleza msukumo wa makubaliano yaliyofikiwa mwezi uliopita kati ya Marekani na Urusi ya kuharibu hazina ya silaha za sumu nchini Syria ifikapo katikati ya mwaka 2014, mjumbe huyo Lakhdar Brahimi amekuwa akisafiri huku na huko katika eneo hilo kutafuta kuungwa mkono kwa kile kinachojulikana kama mazungumzo ya pili ya Geneva.
Upinzani nchini Syria umekataa kuhudhuria hadi pale suala la kujiuzulu kwa utawala wa rais Bashar al-Assad litakapowekwa katika ajenda, dai ambalo linakataliwa na serikali hiyo. Makundi ya waasi yameonya kuwa kushiriki katika mazungumzo hayo kutaonekana sawa na usaliti.
Mkutano hautawezekana
"iwapo upinzani hautahudhuria hakutakuwa na mkutano wa Geneva," Brahimi amesema mjini Damascus siku ya Ijumaa, kabla ya kusafiri kwenda mjini Beirut. Mwanadiplomasia huyo wa siku nyingi raia wa Algeria amekutana na Assad siku ya Jumatano, na kusema serikali ya Syria imekubali kushiriki katika mazungumzo hayo na kwamba upinzani unajaribu kutafuta njia ya kuwakilishwa."
Mzozo huo uliodumu sasa kwa muda wa miezi 31 pia umesababisha mzozo mkubwa wa kibinadamu. Siku ya Ijumaa (01.11.2013), shirika la Umoja wa Mataifa la kutoa misaada ya chakula limeeleza hofu yake juu ya ukosefu mkubwa wa chakula na watoto wakikabiliwa na njaa katika maeneo yaliyozingirwa.
Njaa na utapiamlo
"Shirika la mpango wa chakula duniani linawasi wasi juu ya hatma ya Wasyria wengi ambao wamekwama katika maeneo ya mzozo na bado wanahitaji msaada wa haraka wa chakula," msemaji wa shirika hilo Elisabeth Byrs amewaambia waandishi habari mjini Geneva. "Tunafuatilia ripoti zinazotia hofu zinazotoka miongoni mwa watoto wenye utapiamlo katika maeneo yaliyozingirwa," amesema.
Kuna hali ya ongezeko la idadi ya watoto ambao wanapatiwa matibabu wakiwa na kiwango cha kati na cha juu cha utapia mlo. Wengi wao wamefikishwa katika hospitali mbili za rufaa mjini Damascus," ameongeza msemaji wa shirika la UNICEF Marixie Mercado.
Mamia ya wanawake, watoto na wazee wameondolewa wiki hii kutoka katika mji uliozingirwa wa moadamiyet al-Sham , kusini magharibi ya Damascus.
Maeneo mengi mengine bado yamezingirwa na majeshi tiifu kwa rais Assad , na siku ya Ijumaa wilaya nyingi kati ya hizo katika ukanda wa kusini ya Damascus yalishambuliwa kwa makombora, wamesema wanaharakati. Katika nchi jirani ya Lebanon , shirika la Umoja wa mataifa la kuwahudumia watoto UNICEF , limeripoti siku ya Ijumaa kuwa zaidi ya watoto laki nne ambao ni wakimbizi kutoka Syria wanahitaji haraka msaada , hususan wakati majira ya baridi kali yakikaribia.
"Jumuiya ya kimataifa haiwajibiki tu kutoa misaada ya kiutu kwa watoto lakini pia inawajibu kusaidia juhudi za Lebanon" za kuwasaidia wakimbizi, amesema mkurugenzi wa UNICEF Anthony Lake, ambaye ameitembelea nchi hiyo hivi karibuni.
Wakati huo huo kundi kuu la upinzani la muungano wa kitaifa limesema lina panga kukutana Novemba 9 kuamua iwapo lishiriki katika mazungumzo ya amani ya Geneva, lakini baraza la taifa la Syria , likiwa ni kundi muhimu, limetishia kujitoa iwapo muungano huo utashiriki mazungumzo hayo.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe
Mhariri: Bruce Amani