1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hakuna mkutano bila upinzani wa Syria

1 Novemba 2013

Mjumbe wa amani Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Kiarabu Lakhdar Brahimi amesema leo kuwa kongamano linalopangwa la amani jijini Geneva ili kumaliza vita vya Syria huenda lisiandaliwe bila ya ushiriki wa upinzani.

https://p.dw.com/p/1AA1d
Picha: Reuters

Wakati akikamilisha ziara yake mjini Damascus, Lakhdar Brahimi alitoa wito kwa pande zote mbili, serikali ya Syria na upinzani kuhudhuria mkutano unaopangwa wa amani. Mjumbe huyo wa amani amesema kabla ya kurejea mjini Beirut, kuwa mazungumzo hayo yanayotarajiwa kuandaliwa baadaye mwezi huu jijini Geneva, hayawezi kuendelea kama upinzani Syria utasusia.

Nayo Urusi imesema inataraji kuwa mkutano huo wa amani utaandaliwa kabla ya kumalizika mwaka huu, licha ya tofauti zilizopo na Marekani kuhusu uwakilishi wa upinzani. Waziri Mkuu Dmitry Medvedev ameziomba pande zote katika mzozo wa Syria kulegeza msimamo wakati akiushutumu upinzani kwa kumtaka Rais Bashar al-Assad aondoke kama masharti ya kabla ya mazungumzo.

Ombi la Brahimi na Medvedev, limekuja saa chache tu baada ya maafisa kusema kuwa Israel imefanya shambulizi la kutokea angani katika kituo kimoja cha jeshi la Syria ili kusitisha usafirishaji wa silaha kwa kundi la Hezbollah. Kituo cha televisheni cha Al- Arabiya kimesema kuwa Israel imeipiga kambi ya jeshi la angani la Syria katika mkoa wa Latakia, wakati ikiyalenga makombora ya Urusi yanayotumiwa katika mashambulizi ya ardhini yaliyokusudiwa kupewa kundi la wanambambo wa Hezbollah. Afisa wa Marekani amethibitisha kwa shirika la habari la AFP kuwa “kulikuwa na shambulizi la Israel“ lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu eneo na kilicholengwa, wakati nao maafisa wa Syria wakikataa kuzungumzia habari hizo. Mwezi Mei, Israel ilifanya mashambulizi mawili ya kutokea angani ndani ya Syria, na afisa mmoja wa ngazi ya juu wa Israel akasema mashambulizi hayo mawili yalizilenga silaha zilizoundwa nchini Iran ambazo zilikusudiwa kupewa Hezbollah.

Ndege za Israel zashambulia kambi ya jeshi la Syria
Ndege za Israel zashambulia kambi ya jeshi la SyriaPicha: Jack Gueza/AFP/Getty Images

Hayo yanajiri wakati Shirika la Kupambana na Matumizi ya Silaha za Sumu likisema kuwa silaha zote za sumu nchini Syria zimedhibitiwa. Msemaji wa shirika hilo Michael Luhan amesema “silaha zote zimewekwa katika mifuko ambayo haiwezi kupasuliwa“. Amesema kuna tani 1,000 ya sumu inayoweza kutengeneza silaha, pamoja na tani 290 za silaha za sumu. Shirika hilo pia limesema vifaa vyote vya kutengenezea silaha za sumu vimeteketezwa.

Wakaguzi wana hadi leo kuzuru maeneo yote na kuharibu vifaa vyote vya kutengeneza silaha za sumu kwa mujibu wa muda uliowekwa kwenye azimio la Shirika la OPCW na Umoja wa Mataifa.Katika uwanja wa mapambano, jeshi la Syria limesema majeshi yameutwaa mji wa Sfeira katika mkoa wa Aleppo baada ya kuuzingira kwa siku 27, huku kukiwa na ripoti kuwa waasi wameondoka kabisa katika eneo hilo.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP

Mhariri: Josephat Charo