1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Euro-Gruppe wartet ab

Christoph Hasselbach15 Oktoba 2013

Mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya Euro wamekutana mjini Luxembourg kujadili umoja wa mabenki, lakini hawakuweza kuchukua maamuzi muhimu kutokana na kukosekana kwa waziri wa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/19zXz
Baadhi ya mawaziri wanaoshiriki katika mkutano wa Luxembourg
Baadhi ya mawaziri wanaoshiriki katika mkutano wa LuxembourgPicha: Reuters

Kikao hicho cha mawaziri wote wa fedha kutoka nchi 17 zinazotumia sarafu ya euro kinamkosa mtu mmoja muhimu; waziri wa fedha wa Ujerumani Wolfgang Schäuble ambaye yuko mjini Berlin, akishiriki katika mazungumzo ya kuunda serikali ya mseto. Schäuble ametakiwa na kansela Angela Merkel kuwa karibu ili ashughulikie mahesabu kuhusu gharama ya masuala ambayo chama chake kitalazimika kukubali au kukataa katika majadiliano na vyama vingine.

Kukosekana kwake kumesababisha kuahirishwa uamuzi juu ya vipengele muhimu kuelekea kuundwa kwa umoja wa kibenki. Wapi ifanyike shughuli ya kuzifunga taratibu baadhi ya benki, ni mpango gani unaohitajika kusaidia benki zinazosuasua, na nani atajituisha gharama wakati benki zitakapokuwa bado hazijawekwa chini ya uangaliozi wa Benki Kuu ya Ulaya mwaka ujao? Maswali haya yote hayawezi kujibiwa bila kuwepo kwa waziri wa fedha wa Ujerumani.

Masuala ya kiufundi

Waziri wa fedha wa Uholanzo Jeroen Dijsselbloem amejaribu kuifunika hali hiyo kwa uso wenye tabasamu, akisema kila kitu kinaendelea kama ilivyopangwa. ''Mazungumzo yanajadili masuala ya kiufundi. Wakati mwingine hata wanasiasa wanakabiliwa na hali hiyo, lakini itachukua miezi michache tu'', amesema Dijsselbloem.

Waziri wa fedha wa Uholanzi Jeroen Dijsselbloem, mwenyekiti wa mkutano
Waziri wa fedha wa Uholanzi Jeroen Dijsselbloem, mwenyekiti wa mkutanoPicha: Reuters

Nchi mbili zinazoongoza kiuchumi katika umoja wa euro, Ujerumani na Ufaransa hazikubaliani juu ya namna biashara ya benki zilizofilisika zitakavyoshughulikiwa katika umoja wa kibenki. Ujerumani inapinga mpango wa kuliweka jukumu hilo chini ya Benki Kuu ya Ulaya, bila kuufanyia mabadiliko mkataba wa Ulaya, lakini Ufaransa inasema mabadiliko hayo si lazima, na inaungwa mkono na Halmashauri ya Ulaya.

Kama maridhiano ya misimamo hiyo tofauti, kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na masuala hayo Michel Barnier amependekeza jukumu hilo liuendee mfuko wa uokozi ESM. Pendekezo lake hilo limepingwa na mkuu wa mfuko huo; mjerumani Klaus Regling ambaye ameliambia gazeti la Der Spiegel, kwamba taasisi yake haiko tayari kubeba jukumu hilo gumu.

Matumaini baada ya kipindi kigumu

Habari njema kutoka katika mkutano huo ni kwamba nchi mbili wanachama, Uhispania na Ireland ambazo zilikuwa zikisaidiwa na mpango wa uokozi wa umoja wa sarafu ya euro, zinaweza kuacha kuutegemea mpango huo ifikapo mwakani, kama alivyothibitisha kamishna wa Umoja wa Ulaya ahusikaye na masuala ya uchumi na fedha, Olli Rehn.

Matumaini: Olli Rehn, Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na uchumi na fedha
Matumaini: Olli Rehn, Kamishna wa Umoja wa Ulaya anayehusika na uchumi na fedhaPicha: picture-alliance/dpa

'Ireland na Uhispania zimefanikiwa kuufufua uchumi wao, na ziko katika nafasi nzuri ya kutoka katika mpango wa uokozi hivi karibuni''. Amesema Rehn.

Mkutano wa Mjini Luxembourg hali kadhalika umezungumzia hali katika nchi nyingine wanachama zilizo chini ya mpango wa uokozi, ambazo ni Ugiriki, Ureno na Cyprus. Ugiriki ambayo ndio imepokea fungu kubwa la mpango huo, itahitaji mpango mwingine, lakini uamuzi juu ya hatua hiyo utasubiri hadi mwaka 2014.

Mawaziri wa fedha wa Umoja wa Sarafu ya Euro wamesema mkwamo wa kibajeti unaoikumba Marekani hivi sasa ni kitisho kwa uchumi wa Ulaya, na kuzitaka pande zinazohusika katika mkwamo huo kupata muafaka haraka, ili kuepusha madhara kwa uchumi wa dunia.

Mwandishi: Bernd Riegert

Tafsiri: Daniel Gakuba (DW English Web)

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman