1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mawaziri wa fedha wa umoja wa Ulaya kujadili mzozo wa madeni

13 Septemba 2013

Mawaziri wa fedha wa kanda inayotumia sarafu ya euro wanakutana leo kujadili mzozo wa madeni ambao bado unazikumba nchi kadhaa wanachama huku kukiwa na uwezekano nchi hizo zikahitaji hata msaada zaidi kujikwamua.

https://p.dw.com/p/19gvm
Picha: Peter Muhly/AFP/Getty Images

Mkutano huo wa siku mbili unaofanyika katika mji mkuu wa Lithuania, Vilnius, unatarajiwa kutawaliwa na wasiwasi kuhusu nchi ambazo bado zimezongwa na madeni na uchaguzi mkuu wa Ujerumani ambayo inachukulika kuwa mwamba wa nchi za kanda inayotumia sarafu ya euro kiuchumi.

Uchaguzi huo wa terehe 22 mwezi huu unabashiriwa na wachambuzi wa masuala ya kiuchumi kuzuia maamuzi yoyote kuchukuliwa ya kufadhiliwa au kuidhinishwa kwa mikopo ya uokozi hadi Ujerumani ikamilishe shughuli zake za uchaguzi kwani ni mshikadau muhimu katika masuala ya kiuchumi ya kanda hii.

Ugiriki, Ireland na Ureno, ambazo zote zinamudu kutokana na mikopo ya uokozi, zinatarajiwa kupata msaada hata zaidi katika siku za usoni licha ya kuwa mikopo zaidi imesemekana kutozingatiwa.

Bado nchi kadhaa hazijakuwa imara

Ugiriki ambayo imeshapewa mikopo mara mbili ya uokozi inamulikwa darubini baada ya kubainika kuwa itahitaji mkopo wa tatu ambao unaonekana mwiko wa kiasi ya euro bilioni 10 ili kupiga jeki uchumi wake unaotetereka.

Waziri wa maendeleo wa Ugiriki Kostis Hatzidakis
Waziri wa maendeleo wa Ugiriki Kostis HatzidakisPicha: picture-alliance/dpa

Mawaziri hao wa fedha pia wataiangalia kwa makini Ireland ambayo mpango wake wa uokozi unakamilika mwishoni mwa mwaka huu na inatarajia kuungwa mkono kifedha inapojizatiti kurejea katika hali yake ya kawaida ya kuzalisha uchumi wake kupitia masoko ya hisa.

Ureno nayo imejipata mashakani baada ya sehemu ya mpango wake wa uokozi kutangazwa kuwa kinyume cha sheria na kuiacha serikali ikiwa inatapatatapa na kutafuta njia mbadala za kuweka mambo yake sawa kiuchumi.

Slovenia pia imegonga vichwa vya habari wiki hii baada ya gazeti la Ujerumani, Handelsblatt, kuripoti kuwa benki kuu ya Ulaya, ECB, inaishinikiza nchi hiyo kugeukia mfuko wa uokozi ili kusaidikia. Slovenia imekuwa ikipita taabu kulainisha sekta yake ya benki, matatizo ambayo pia yanaikumba Cyprus ambayo inatafuta mkopo mwingine wa uokozi.

Kamishna wa masuala ya kiuchumi wa umoja wa Ulaya, Olli Rehn, hajaisaza Ufaransa pia katika nchi zinazohitajika kujiimarisha hata zaidi kiuchumi. Rehn amesema nchi hiyo sharti iendeleze mipango yake ya kufanyia marekebisho uchumi wake ili irejee katika nafasi yake ya kutoa ushindani.

ECB kuwa msimamizi pekee

Hapo jana, wabunge wa Umoja wa Ulaya walikubaliana kuhusu hatua ya kwanza katika mpango mkubwa wa kuimarisha udhibiti wa mabenki kwa kuipa benki kuu ya Ulaya, ECB, mamlaka ya kuyadhibiti mabenki makubwa katika kanda ya sarafu ya euro katika kipindi cha mwaka mmoja.

Kamishna wa masuala ya kiuchumi wa umoja wa Ulaya Olli Rehn
Kamishna wa masuala ya kiuchumi wa umoja wa Ulaya Olli RehnPicha: picture-alliance/dpa

Hatua hiyo ambayo ni nguzo ya kwanza katika mpango mpana unaolenga kuweka usalama na uwazi katika mabenki ulipigiwa kura jana ili kuifanya ECB msimamizi pekee wa mabenki.

Nguzo ya pili katika mpango wa muungano wa mabenki inayofahamika kama utaratibu wa pamoja ambao utaipa mamlaka halmashauri hiyo kuifunga benki yoyote ya kanda ya euro itakayofeli.

Mawaziri wa fedha wa kutoka Umoja wa Ulaya ambao sio wanachama wa nchi zinazotumia sarafu ya euro wataungana na wenzao hao hapo kesho wakioongozwa na Uinegereza ambayo haina hakika iwapo inataka kujiunga na mpango huo wa benki zote kusimamiwa na benki ya Ulaya.

Mwandishi:Caro Robi/dpa/afp

Mhariri: Josephat Charo