1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden,Lapid wasaini mkataba mpya dhidi ya Iran

Daniel Gakuba
14 Julai 2022

Rais wa Marekani Joe Biden, pamoja na mwenyeji wake wa Israel, Waziri Mkuu wa Israel Yair Lapid, wametia saini mkataba mpya wa kiusalama unaoimarisha dhamira ya pamoja ya kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia.

https://p.dw.com/p/4E9Ge
Joe Biden und Yair Lapid | Jerusalem, Israel
Picha: Atef Safadi/AP/picture alliance

Rais wa Marekani Joe Biden aliyeko ziarani nchini Israel, pamoja na mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Israel Yair Lapid, wametia saini mkataba mpya wa kiusalama unaoimarisha dhamira ya pamoja ya kuizuia Iran kuunda silaha za nyuklia.

Baada ya kuutia saini mkataba huo mjini Jerusalem, Rais Biden ameahidi kuwa Marekani itatumia nguvu zake zote kuuhakikisha kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kamwe haizipati silaha za nyuklia.

Biden ameusifu mkataba huo, akisema una maslahi mapana nje ya Israel,Marekani na ulimwengu mzima, huku akisisitiza kuwa anaendelea kuamini diplomasia ndiyo njia bora ya kuhakikisha hilo.

"Tutaendelea kushirikiana na Israel kukabili vitisho vya Iran kwenye ukanda wote" Alisema

katika hotuba yake alionekana kulaani vikali vitendo vya kuunga mkono magaidi, mipango ya makombora ya masafa marefu, na kuyapa silaha makundi ya kigaidi inayoyatumia kama Hezbollah.'

Soma pia:Biden, Yair wakubaliana kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran

Mwaka 2015, mataifa yenye nguvu yakiongozwa na Marekani yalifikia makubaliano juu ya mkataba wa nyukilia wa Iran, lakini mtangulizi wa Biden, Rais Donald Trump aliiondoa Marekani katika makubaliano hayo mwaka 2018.

Israel yafurahishwa na mkataba huo dhidi ya Iran

Hivi sasa juhudi zinaendelea kuyafufua makubaliano hayo, lakini Biden amesema kuwa ingawa Marekani inaunga mkono juhudi hizo haitasubiri milele ridhaa ya Iran.

Marekani yaanza kutekeleza vikwazo vipya dhidi ya Iran

Waziri mkuu wa Israel Yair Lapid ameonekana mwenye furaha kusainiwa kwa mkataba na Marekani wa kuibana Iran, akisema maneno matupu na diplomasia haviwezi kuishawishi Iran kuachana na azma yake ya kupata silaha za atomiki.

Hapo jana, Rais wa Iran Ebrahim Raisi alikejeli ziara ya Biden nchini Israel, akisema ikiwa malengo yake ni kupigia debe usalama wa taifa hilo la kiyahudi katika eneo la mashariki ya kati, malengo hayo yataambulia patupu.

Soma pia:Biden awasili Jerusalem kuanza ziara ya Mashariki ya Kati

Shughuli nyingine kwenye ratiba ya Rais Joe Biden leo ilikuwa mkutano kwa njia ya vidio na viongozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu, UAE, India na Israel, ambao pamoja na Marekani wanaunda ushirika unaojulikana kama I2U2.

Ushirika huo ulianzishwa mwaka jana mjini Washington katika mazungumzo yaliyofanyika nyumbani kwa balozi wa UAE.

Waziri Mkuu wa Israel Yair Lapid amesema yalitokana na dhana kuwa yeyote anayetambua kuwa tunaishi katika dunia mpya yenye aina mpya ya changamoto, atastawi na kufanikiwa.

Jioni hii Biden amepangiwa kukutana na rais wa Israel Isaac Herzog na pia waziri mkuu wa zamani Benjamin Netanyahu, na hapo kesho atazungumza na kiongozi wa mamlaka ya Wapalestina Mahmoud Abbas kabla ya kuelekea Saudi Arabia.