1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri wa mambo ya nje wa Israel aizuru UAE

Saleh Mwanamilongo
29 Juni 2021

Waziri wa Mambo ya Nje wa Israel, Yair Lapid amewasili Abu Dhabi ikiwa ni ziara ya kwanza ya afisa wa ngazi ya juu wa Israel kulizuru taifa hilo la Umoja wa Falme za Kiarabu.

https://p.dw.com/p/3vkm4
Vereinigte arabische Emirate | Israels Außenminiter Yair Lapid zu Besuch in Abu Dhabi
Picha: Shlomi Amsalem/Government Press Office/Reuters

Ziara hiyo inafanyika tangu nchi hizo mbili ziliporejesha uhusiano wa kidiplomasia miezi tisa iliyopita. 

Waziri Yair Lapid anatarajiwa kuwa na mazungumzo na mwenzake wa Umoja wa Famle za Kiarabu Sheikh Zayed Al Nahyan. Mazungumzo hayo yatahusu hasa Iran, ambayo imechukuliwa na nchi hizo mbili kama kitisho cha kanda hiyo.

Serikali za Umoja wa Falme za Kiarabu na ile ya Isreal zina mashaka na mktaba wa nyuklia baina ya Iran na nchi zenye nguvu duniani uliofikiwa mwaka 2015 chini ya utawala wa rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama.

Wasiwasi wa nchi hizo mbili kuhusu Iran,ulisababisha kuweko na mikutano ya siri kabla ya kurejesha uhusiano wao wa kidiplomasia mwaka uliopita.

VAE | Besuch Yair Lapid | israelischer Außenminister
Yair Lapid akiwa na viongozi wa viongozi wa Abu DhabiPicha: Israeli Prime Ministry/AA/picture alliance

Rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump akiungwa mkono na Waziri Mkuu wa zamani wa Israel Benjamin Netanyahu aliiondoa Marekani kwenye mkataba wa nyuklia na Iran mwaka 2018 na kuiwekea Iran vikwazo vya kiuchumi.
Mkataba wa kurejeshwa kwa mahusiano baina ya Isreal na Umoja wa Famle za Kiarabu ulisaidiwa na utawala wa Trump.

Netanyahu na Trump waliupongeza mkataba huo na kuuita kuwa moja ya mafanikio makubwa ya uongozi wao.

Mkataba wa kuimarisha uhusiano

Umoja wa Falme za Kiarabu na Isreal walitia saini mkataba uliojulikana kama "Abraham Accords", hatua iliyofuatiwa baadaye na Bahrain katika kuboresha mahusiano yake na Isreal. Nchi hizo mbili za Kiarabu zilirejesha mahusiano na Isreal baada ya Misri na Jordan. Baadaye Sudan na Morocco zilichukuwa pia hatua kama hiyo.

Utawala wa Rais Joe Biden uliunga mkono mikataba hiyo lakini ulisema haichukuwi nafasi ya juhudi za ufumbuzi wa mzozo baina ya WaIsrael na Wapalestina.

Biden alishinikiza pia kufufua mkataba wa nyuklia wa Iran na nchi zenye nguvu duniani,ambao unalenga kuizuwia Iran kutengenza silaha za nyuklia.
Jumapili, Lapid alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken mjini Roma, Italia, na baadaye waziri wa mambo ya nje wa Bahrain.

Vereinigte arabische Emirate | Israels Außenminiter Yair Lapid zu Besuch in Abu Dhabi
Yair Lapid akiuzindua ubalozi wa Israel huko Abu DhabiPicha: Shlomi Amsalem/Government Press Office/Reuters

Alinukuliwa akisema kuwa Israel ina mashaka makubwa na mazungumzo ya Vienna kuhusu mkataba huo wa nyuklia, lakini alielezea kuwa Israel itatoa vipingamizi vyake kwa njia ya faragha.

Wakati wa ziara yake Jumanne, Lapid ameuzindua ubalozi wa Israel mjini Abu Dhabi.

Lapid na maonesho ya biashara

Wizara ya mambo ya nje ya Israel ilisema kuwa Lapid atahudhuria pia soko la maonyesho ya biashara ambako makampuni ya Israel yataonyesha vifaa vya teknolojia.

Siku ya Jumatano, Yair Lapid anatarajiwa kuzindua ubalozi mdogo wa Israel mjini Dubai. Atakutana pia na jamii ya Wayahudi wanaoishi mjini Dubai.

Ziara hiyo ya waziri wa mambo ya nje wa Isreal mjini Abu Dhabi imekuja wiki sita baada ya vita vya siku 11 baina ya Isreal na wanamgambo wa Hamas katika ukanda wa Gaza ambavyo vilisababisha  vifo vya Wapalestina 254. Nchini Isreal vita hivyo vilisababisha vifo vya Waisrael 13.

(AP)