Biden: Sikubaliani na mbinu za Netanyahu huko Gaza
10 Aprili 2024Akizungumza katika televisheni ya Network Univision inayotangaza kwa lugha ya Kihispaniola, Rais Biden amesema anachokifanya Netanyahu ni makosa na kwamba hakubaliani na mbinu anazozitumia. ''Sikubaliani na mbinu anazotumia. Hivyo natoa wito kwa Israel kusitisha mapigano na kuruhusu upelekwaji wa misaada ya chakula na dawa huko Gaza, katika wiki sita, au nane zijazo. Nimezungumza na kila mmoja kuanzia viongozi wa Saudi Arabia hadi Jordan na Misri. Wako tayari kupeleka chakula huko. Na nadhani hakuna kisingizio cha kutopeleka dawa na chakula kwa watu hao. Inapaswa kufanyika sasa,'' alisisitiza Biden.
Uturuki yaiwekea Israel vikwazo vya kibiashara
Akitilia mkazo kuhusu kubadilika kwa msimamo wake hivi karibuni, katika mahojiano hayo yaliyofanywa Aprili 3, siku mbili baada ya Israel kuwashambulia wafanyakazi saba wa mashirika ya kutoa msaada huko Gaza, na kuchapishwa Jumanne usiku, Biden amesema Israel inapaswa pia kuziruhusu nchi nyingine katika ukanda huo kusaidia kusambaza misaada.
Wakati huo huo, Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant, amesema bado hakuna tarehe rasmi iliyopangwa kwa ajili ya kufanya mashambulizi ya ardhini huko Rafah. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti za vyombo vya habari vya Axios, Haaretz na The Times la Israel. Akizungumza na waziri mwenzake wa Marekani, Lloyd Austin, Gallant amesema Israel bado iko katika mchakato wa kupanga kuwaondoa raia.
Marekani yaipinga Israek kufanya mashambulizi makubwa
Ikiwa matamshi ya Gallant yatathibitishwa, yatakinzana na kauli ya awali ya Netanyahu ambaye mara kwa mara amekuwa akisema mashambulizi ya Rafah yataendelea licha ya kukosolewa kimataifa. Netanyahu, ambaye anakabiliwa na shinikizo kutoka kwa wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia, alikuwa ametangaza kukamilika kwa mashambulizi yaliyopangwa huko Rafah, ambako zaidi ya Wapalestina milioni moja wamekimbilia.
Blinken amesema Marekani imekuwa ikipinga mipango ya Israel kufanya mashambulizi makubwa, ikisema itayaweka maisha ya raia hatarini. Maafisa wa Marekani wanatarajia kukutana na ujumbe wa Israel wiki ijayo kujadiliana kuhusu uamuzi huo.
Cameron awasili Washington kujadiliana Ukraine, Gaza
Huku hayo yakijiri, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez, ameonya kuwa namna Israel inavishughulikia vita dhidi ya Hamas huko Gaza vinaweza kuliyumbisha eneo la Mashariki ya Kati, na kwamba ni kitisho kwa ulimwengu mzima. Akizungumza siku ya Jumatano bungeni, Sanchez amesema kutambuliwa kwa taifa la Palestina ni kwa ''maslahi ya kijiografia ya Ulaya." Amesema jumuiya ya kimataifa haiwezi kulisaidia taifa ya Palestina, ikiwa haiwezi kutambua kuwepo kwake.
Ama kwa upande mwingine kiongozi mkuu wa kidini wa Iran, Ayatollah Ali Khamenei amesisitiza ahadi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel kutokana na mauaji ya majenerali wa Iran nchini Syria. Matamshi hayo ameyatoa siku ya Jumatano wakati wa Swala ya sikukuu ya Eid al-Fitr, akisema kuwa shambulizi la anga lililoharibu ubalozi mdogo wa Iran nchini Syria mapema mwezi huu, yalikuwa ni makosa, na ni sawa kufanya shambulizi katika ardhi ya Iran.
(AFP, AP, Reuters)