Biden na Starmer wakutana Washington kuijadili Ukraine
14 Septemba 2024Waziri Mkuu wa Uingereza Kier Starmer ameitembelea Ikulu ya White House na kuzungumza na Rais wa Marekani Joe Biden kuhusu hatua zinazofuata katika vita vya Ukraine na Urusi.
Starmer alisema kuwa awamu inayofuata ya Ukraine katika mapigano yake na Urusi inaweza kuwa "muhimu zaidi", huku akiongeza kuwa kwa sasa yapo matukio mengi yaliyopo mbele yao na Marekani pia ikiwa inajiandaa kwa uchaguzi wa rais hapo baadaye mwaka huu.
Soma zaidi. Biden, Starmer waahirisha uamuzi wa makombora ya Ukraine
Lakini licha ya uvumi kabla ya mkutano huo juu ya uwezekano wa mabadiliko ya msimamo wa Marekani na Uingereza kuhusu Ukraine kutumia silaha zao za masafa marefu kushambulia maeneo ya ndani ya Urusi, Marekani ilionesha kutobadili msimamo wake juu ya vita hivyo.
Kwa upande mwingine, Urusi imeonya kuwa kuiruhusu Ukraine kutumia silaha za masafa marefu kutaitumbukiza NATO katika vita vya moja kwa moja na Urusi.