Biden amualika Trump katika Ikulu ya White House
7 Novemba 2024Makamu wa Rais Kamala Harris akikubali kushindwa katika kinyang'anyiro hicho lakini akiahidi kwamba bado mapambano yanaendelea.
Kwa mujibu wa msemaji wa timu ya kampeni ya Trump, Steven Cheung, Biden alimpigia simu Trump kumpongeza kwa ushindi huo na kumualika kutembelea Ikulu ya White House ili kuratibu makabidhiano ya madaraka.
Ikumbukwe kwamba Trump alishindwa katika uchaguzi wa rais wa 2020 kwa Biden, matokeo ambayo hadi leo amekuwa akiyapinga na alikataa kushiriki kwenye sherehe ya kuapishwa kwa Biden tofauti na ilivyokuwa desturi ya Marekani.
Soma pia:Trump arejea Ikulu ya White House kwa ushindi wa kushangaza
Biden anatarajiwa kutoka hotuba kwa taifa leo Alhamisi, akiahidi kukabidhi madaraka kwa amani kwa Trump baada ya adui wake huyo wa kisiasa kupata ushindi mkubwa dhidi ya makamu wake, Kamala Harris.
Harris akubali kushindwa
Akizungumza katika chuo kikuu cha Howard jana Jumatano alasiri, Harris alikubali kushindwa na kuwafariji wapiga kura waliokuwa na matumaini kwamba angekuwa mwanamke wa kwanza kuiongoza Marekani.
Harris alisema amempigia simu Trump kumpongeza na aliahidi kusaidia kipindi cha mpito, ingawa wakati huo huo akiongeza kusema kwamba mapambano yanaendelea:
"Hatutaacha kamwe kupigana kulinda shule zetu na mitaa yetu dhidi ya mashambulizi ya silaha. Na Wamarekani hatutaacha kamwe kupigania demokrasia yetu, kwa utawala wa sheria, kwa haki sawa, na kwa wazo adhimu ambalo kila mmoja wetu, haijalishi sisi ni nani au tunaanzia wapi, kwamba ana haki fulani za kimsingi na uhuru ambao lazima uheshimiwe na kuzingatiwa."
Muelekeo wa mahusiano ya Marekani
Ushindi mkubwa wa Trump katika kinyang'anyiro cha urais unaleta enzi mpya ya sintofahamu nchini Marekani na duniani kote, na kuashiria mabadiliko kwenye uhusiano wa taifa hilo kubwa na mataifa mengine ikiwemo China, ambayo imekuwa katika miaka ya hivi karibuni imekuwa na mivutano ya kibiashara na juu ya hadhi ya kisiwa cha Taiwan.
Katika ujumbe wake kwa Trump, Rais wa China Xi Jinping amesema Beijing na Washington lazima zitafute njia ya "kuelewana", akisisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa ingetarajia mataifa hayo mawili "kuheshimiana na kuishi pamoja kwa amani".
Iran nayo ambayo pia imekuwa na uhusiano mbaya na Marekani wakati wa utawala wa Trump, imeutaja ushindi wa Trump katika uchaguzi wa rais wa Marekani kuwa fursa kwa Marekani kutathmini upya kile ilichokiita "sera mbovu".
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje yaIran Esmaeil Baghaei amenukuliwa na kituo cha habari cha kitaifa akisema Iran ina uzoefu mchungu sana na sera na mbinu za serikali tofauti za Marekani.
Kurudi kwa Trump katika Ikulu ya White House pia, kutafunika mkutano wa siku mbili wa viongozi wa Ulaya huko Budapest, Hungary. Awali mazungumzo yalipangwa kushughulikia uchumi, uhamiaji,
uchaguzi wa hivi majuzi huko Georgia, mzozo unaoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati, na uvamizi kamili wa Urusi wa Ukraine.