1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden aapishwa kuwa rais: 'Demokrasia imeshinda'

20 Januari 2021

Joe Biden ameapishwa kuwa rais wa 46 wa Marekani, na kutangaza kuwa demokrasia imeshinda na kuwasihi Wamarekani kuungana na kupambana na migogoro ya kihistoria inayolikumba taifa hilo lililogawika.

https://p.dw.com/p/3oCn8
USA Washington | Amtseinführung: Joe Biden
Picha: Rob Carr/Getty Images

Biden alikula kiapo nje ya jengo la bunge – Capitol ambalo lilivamiwa wiki mbili zilizopita na umati wa wafuasi wa rais aliyeondoka Donald Trump. Sherehe ya kuapishwa Biden ilifanywa chini ya ulinzi mkali na kuhudhuriwa na wageni wachache walioalikwa kutokana na janga la virusi vya corona.

Soma pia: Biden kuapishwa rais wa 46 wa Marekani

Katika hotuba yake baada ya kula kiapo cha rais, Biden alisema nia ya watu imesikika, na nia ya watu imetimizwa. “Tumejifunza tena kuwa demokrasia ni kitu cha thamani, na demokrasia ni dhaifu. Kwa wakati huu, rafiki zangu, demokrasia imeshinda.“ Alisema Biden

USA Washington | Inauguration | Kamala Harris
Kamala Harris aweka historiaPicha: Brendan Smialowski/AFP/Getty Images

Biden hakumtaja mtangulizi wake, ambaye alikiuka utamaduni wa marais waliopita na kuondoka mjini Washington kabla ya sherehe hiyo, lakini hotuba yake ilionekana wazi kumkashifu Trump.

Rais mpya alilaani “uongo unaoenezwa kwa ajili ya madaraka na faida“ na akaeleza wazi changamoto zilizopo mbele yao.

Kutokuwepo kwa mtangulizi wa Biden katika sherehe ya kuapishwa kwake kulidhihirisha mpasuko wa kitaifa unaopaswa kuzibwa.

Lakini marais watatu wa zamani wa kutoka pande mbili za kisiasa – Bill Clinton, George W. Bush na Barack Obama – walikuwepo kushuhudia makabidiano ya heshima ya madaraka.

Trump, anayesubiri kesi yake ya pili ya kushitakiwa bungeni, alikuwa katika makazi yake ya kifahari ya Florida katika wakati ambao hafla hiyo ya kula kiapo ilikuwa ikiendelea.

Akiwa na umri wa miaka 78, Biden ndiye rais mkongwe zaidi kuapishwa Marekani. Historia Zaidi iliandikwa kando yake, wakati Kamala Harris alikuwa mwanamke wa kwanza kuwa makamu wa rais.

Washington scheidender Präsident Donald Trump
Trump hakuhudhuria kuapishwa kwa BidenPicha: Manuel Balce Ceneta/AP/picture alliance

Seneta huyo wa zamani wa Marekani kutoka California pia ni mtu wa kwanza mweusi na mtu wa kwanza wa asili ya Kusini mwa Asia kuchukua wadhifa wa makamu wa rais na mwanamke wa ngazi ya juu kabisa kuwahi kuhudumu serikalini.

Viongozi wakuu wa Republican, akiwemo Makamu wa Rais Mike Pence na wajumbe wa chama hicho bungeni, hawakuonekana hafla ya kumuaga Trump na badala yake wakahudhuria sherehe ya kuapishwa Biden.

Soma pia: Trump aondoka rasmi ikulu kwa mara ya mwisho kama rais

Katika hafla ndogo iliyoandaliwa katika uwanja wa ndege wa Joint Base Andrews, alipanda ndege ya Air Force One kwa mara ya mwisho kama rais.

“Nitawapigania wakati wote. Nitafuatilia. Nitasikiliza na nitawaambieni kuwa mustakabali wa nchi hii ni mzuri sana”. Alisema Trump. Aliitakia mafanikio serikali mpya lakini hakulitaja jina la Biden.

Trump lakini alitimiza utamaduni kwa kumuachia Biden ofisini barua aliyomuandikia kabla ya kuondoka.

	USA | Washington | Inauguration | Joe Biden im Oval Office
Biden tayari amesaini amri kadhaa za kiutendajiPicha: Jim Watson/AFP

Baadaye mchana, Biden alihudhuria hafla ya kuweka shada la maua kwenye Kaburi la Mwanajeshi Asiyejulikana, katika makaburi ya Kitaifa ya Arlington jimboni Virginia, akiandamana na Obama, Bush na Clinton.

Kisha msafara wake ukaeleeka katika White House. Biden na familia yake walishukia barabarani na kutembea kwa miguu umbali wa mita kadhaa kuelekea katika makazi yake mapya.

Biden ameanza kazi kwa kusaini maagizo kadhaa ya kiutendaji kuhusu masuala ambayo hayahitaji idhini ya bunge ikiwemo kuirejesha Marekani katika mkataba wa Paris wa mabadiliko ya tabia nchi.

Viongozi wa ulimwengu walituma salamu za pongezi, huku washirika kadhaa wa Marekani wakielezea ahueni katika kuapishwa kwa Biden, baada ya muhula usiotabirika wa Trump ambao uliangazia ajenda ya “Marekani Kwanza”.

afp,ap, reuters, dpa