1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden kuapishwa chini ya ulinzi mkali

20 Januari 2021

Rais mteule Joe Biden alielekea Washington katika mkesha wa sherehe ya kuapishwa kwake, wakati mtangulizi wake Donald Trump ambaye atasusia hafla hiyo ya kula kiapo – kwa mara ya kwanza akiitakia mafanikio serikali mpya

https://p.dw.com/p/3o9L9
USA | Washington I Amtseinführung | Joe Biden
Picha: Carolyn Kaster/AP Photo/picture alliance

Machozi yalimtoka Biden katika sherehe ya kumuaga katika mji wa nyumbani wa Wilmington, Delaware, ambako alitoa heshima kwa marehemu mwanawe wa kiume kabla ya kupanda ndege kuelekea katika mji mkuu.

Soma pia: Biden kusaini maagizo ya kiutendaji baada ya kuapishwa

Trump, kwa upande wake ambaye hajaonekana hadharani kwa wiki moja sasa, alivunja ukimya wake wa siku nyingi kupitia hotuba iliyorekodiwa kwenye mkanda wa video.

Symbolbild USA Trump Abschied
Trump aitakia mafanikio serikali ya BidenPicha: Carlos Barria/REUTERS

Trump kwa mara ya kwanza aliiwaomba Wamarekani "kuiombea" mafanikio serikali ijayo ya Biden -- ikiwa ni mabadiliko ya msimamo wa wiki nyingi alizotumia kuishawishi idadi kubwa ya wafuasi wake wa Republican kuwa Mdemocrat huyo alifanya udanganyifu katika kinyang'yiro cha urais.

Trump bado hajampongeza binafsi Biden kwa ushindi wake wala kumualika kwa utamaduni wa kikombe cha chai katika Ofisi yake ya Ikulu.

Nje ya uzio wa Ikulu ya White House, katikati ya mji wa Washington umechukua muonekano mpya kabla ya kuapishwa kwa Biden, ukiwa na wanajeshi wengi wa Ulinzi wa Taifa na kwa kiasi kikubwa bila watu wa kawaida.

USA | Washington | Gedenken an die Opfer der Coronavirus-Pandemie im Lincoln
Biden na wenzake wawakumbuka wahanga wa coronaPicha: Chip Somodevilla/AFP/Getty Images

Vizuizi vya janga la corona vina maana kuwa sherehe ya kuapishwa leo saa sita mchana saa za Marekani itahudhuriwa na wageni wachache mno. Lakini hofu ya mashambulizi ya watu wa siasa za mrengo wa kulia kufuatia vurugu za kumuunga mkono Trump zilizotokea katika jengo la bunge la Capitol mnamo Januari 6 imechochea hatua ya isiyo ya kawaida ya kupelekwa wanajeshi wengi, vizuizi vya saruji na kuyatenga maeneo salama.

Biden na mkewe Jill, pamoja na makamu wa rais Kamala Harris – ambaye ni mwanamke wa kwanza katika historia kushika wadhifa huo – kwanza walihudhuria hafla ya kumbukumbu katika Bwawa lililopo kwenye Makumbusho ya Lincoln kuwakumbuka Wamarekani 400,000 waliouawa mpaka sasa kutokana na ugonjwa wa Covid-19.

Eneo ambalo Biden ataapishwa limewekwa bendera 200,000 za Marekani kuwakilisha umati mkubwa wa wartu ambao kawaida huhudhuria sherehe hizo za kiapo. Minara 56 ya nuru itawashwa kuwakilisha majimbo ya Marekani na mikoa. Wanajeshi 20,000 wa ulinzi wa taifa wameshika doria, wengi wao wakiwa na bunduki za rashasha na kuvalia sare kamili za kijeshi.

	USA | Washington | US-Kapitol vor der Amtseinführung des gewählten US-Präsidenten Joe Biden
Askari wa Ulinzi wa Taifa wameweka doria WashingtonPicha: Rebecca Blackwell/AP Photo/picture alliance

Lakini Biden anaingia na ujumbe mzito wa umona, akisisitiza kuwa anaweza kuileta pamoja nchi iliyogawika na kuikabili mizozo kadhaa inayolikumba taifa hilo, kwa kuanza na corona.

Hotuba yake itadumu dakika 20 hadi 30 na itawalenga Wamarekani wote kuungana katika kupambana na changamoto za nchi.

Soma pia: Bunge la Marekani lapitisha mashtaka ya Trump mara ya pili

Kwa Trump, miongoni mwa mambo ya mwisho kuyafanya kabla ya kuondoka ni kuwasaheme wafungwa 100. Aidha ameamuru kutolewa kwa nyaraka za siri zinazohusiana na uchunguzi wa muda mrefu wa shirika la upelelezi la FBI dhidi ya Urusi wa kampeni yake ya urais mwaka wa 2016.

afp, dpa, ap, reuters